IQNA

Katika mkutano Vatican, Iran yatoa wito kwa Kanisa Katoliki kuchukua hatua kukomesha mauaji ya kimbari Gaza

21:18 - May 24, 2025
Habari ID: 3480732
IQNA-Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, katika mkutano na maafisa wa Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani, Vatican huko mjini Rome, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kimataifa kukomesha uhalifu unaoendelea kutendwa na utawala katili wa Israel huku Gaza, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika katika eneo hilo lililozingirwa.

Araghchi ambaye alikuwa mjini Rome kuhudhuria duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, jana Ijumaa alikutana na Kadinali Pietro Parolin, Waziri Mkuu wa Vatican.

Askofu Mkuu Paul Gallagher, Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican pia alihudhuria mkutano huo. Araghchi alitoa salamu za rambirambi kwa kuaga dunia Papa Francis na kupongeza kuchaguliwa kwa Papa Leo wa 14 kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alitaja hatua ya Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina, na vitendo vyake vya ubaguzi wa rangi, na ukiukaji mkubwa wa haki za msingi za watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na haki yao ya kujitawala, kama sababu kuu za ukosefu wa usalama na matatizo katika eneo la Asia Magharibi.

Aragchi alisisitiza kwamba, ikizingatiwa kuwa suluhisho la mataifa mawili, kwa miongo kadhaa, limekuwa ahadi isiyoweza kutekelezeka ambayo imesababisha kuongezeka kwa kunyimwa haki za Wapalestina, na kwa kuzingatia juhudi za utawala wa Israeli za kufuta uwepo wa Palestina kwa njia ya ukoloni, suluhisho lililopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuundwa kwa taifa moja la kidemokrasia katika ardhi yote ya Palestina, ambalo litapatikana kupitia kura ya maoni inayoshirikisha wakazi wa asili wote wa Palestina – Waislamu, Wayahudi, na Wakristo vilevile.

Wakati wa mkutano huo, Araghchi alielezea msimamo wa Iran kuhusu matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na kuwafahamisha maafisa wakuu wa Vatican kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Iran na Marekani.

Wakati huo huo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Italia katika mazungumzo yao kwa njia ya simu wamezungumzia matukio ya hivi punde katika eneo la Magharibi mwa Asia hususan kuendelea mauaji ya kimbari huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kusisitiza juu ya haja ya kuchukuliwa hatua za dharura za kukomesha mauaji hayo na kutoa msaada kwa watu waliokimbia makazi yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye ameenda Rome kushiriki duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani, alipokea simu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, ambaye yuko nje ya nchi, na kumjulisha kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo ya Ijumaa.

3493210

Habari zinazohusiana
captcha