IQNA

Diplomasia

Iran yaitaka Marekani isitishe vita vya Israel dhidi ya Gaza, Lebanon

17:02 - November 11, 2024
Habari ID: 3479738
IQNA - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utawala wa Marekani unaomaliza muda wake unatarajiwa kutumia muda uliobakia madarakani kukomesha hujuma za Israel huko Gaza na Lebanon.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran siku ya Jumatatu, Esmaeil Baghaei amesema utawala wa Biden utaacha historia ya kutisha kwa uungaji mkono wake wa dhati kwa utawala wa Israel.

Baghaei ameongeza kuwa, jumuiya ya kimataifa inatarajia Washington itazuia ongezeko la ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi.

Kwingineko Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utendaji wa Marekani kuhusu masuala ya kieneo na jinai za utawala wa Israel huko Gaza na Lebanon pamoja na sera zake kuhusu Iran ni muhimu zaidi kuliko matokeo ya uchaguzi wa nchi hiyo.

Amesema: "Sote tunajua kwamba sababu kuu za kuendelea na kupanuka jinai za utawala wa Kizayuni ni uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huu, kutuma silaha na kuzuia kupitishwa azimio lolote dhidi ya utawala huu katika majukwaa ya kimataifa."

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameelezea matumaini yake kuwa utawala mpya wa Marekani utazuia kuongezeka kwa vita na kwamba viongozi wa Marekani wajifunze kutokana na hali inayoendelea katika eneo na kushikamana na ahadi zao.

Akijibu swali kuhusu madai ya kuhusika kwa Iran katika njama ya kuwaua maafisa wa zamani na wa sasa wa Marekani, akiwemo Rais Mteule Donald Trump, Baghaei amesema inasikitisha kwamba maafisa wa Marekani wanatumia muda na nguvu zao kutoa madai ambayo hayana msingi wowote.

Kuhusu jinai za utawala wa Israel, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utawala wa Israel umekuwa ukitumia sayansi na teknolojia katika miaka ya hivi karibuni kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

3490647 

Habari zinazohusiana
captcha