China imeitaka mahakama ya ICC kuwa na utendaji wa haki katika maamuzi yake na kukosoa undumakuwili wa baadhi ya mataifa ya dunia kuhusiana na uhalifu na jinai za kivita.
Lin Jian, msemaji katika Wizara ya mambo ya kigeni ya China, ameishutumu Marekani kwa kutokuwa na msimamo kuhusu suala la ICC, ambapo inapinga kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu, lakini uunga mkono kukamatwa kwa rais wa Russia Vladimir Putin.
Stéphane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaheshimu utendaji na mamlaka ya mahakama hiyo.
Josep Borrell Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema: Amri ya Mahakama ICC dhidi ya Netanyahu na Gallant sio ya kisiasa na uamuzi huo lazima uheshimiwe na kutekelezwa.
Uswisi, Uholanzi na Ubelgiji sambamba na kupongeza uamuzi huo zimetangaza kuwa, zitamtia mbaroni Netanyahu endapo atakwenda katika mataifa hayo.
Waziri Mkuu wa Canada na Waziri wa Ulinzi wa Italia wamesifu uamuzi huo na kueleza kwamba, hiyo ni hatua ambayo wao walikuwa wakiitaka tangu awali.
Rais wa Colombia amesema kuwa, Netanyahu ametenda jinai za kivita na mahakama ya ICC imethibitisha hilo hivyo ni lazima kuheshhimu uamuzi huo.
Msimamo wa Afrika Kusini
Serikali ya Afrika Kusini imepongeza hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kutoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu,pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema kutolewa kwa hati ya kuwakamata watenda jinai hao wa Israel ni jambo la busara kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu huko Gaza. Afrika Kusini, ambayo imewasilisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), imesisitiza kuendelea kujitolea kwake kuheshimu sheria za kimatifa na kutaka mataifa ambayo ni wanachama kutekeleza majukumu yao kulingana na utaratibu uliowekwa na sheria za Roma wa kuwakamata watenda jinao hao wa Israel.
Kauli kutoka Marekani
Seneta wa Marekani Bernie Sanders ameunga mkono uamuzi uliotoloewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC jana Alkhamisi wa kuamuru kukamatwa Netanyahu na Gallant.
Sanders ameeleza katika taarifa kwamba mashtaka ya ICC "yana msingi mzuri," akisisitiza umuhimu wa Mikataba ya Geneva, ambayo iliundwa kulinda raia na kuzuia vitendo visivyo vya kibinadamu wakati wa vita.
Seneta huyo wa Marekani amesema, mashtaka ya ICC dhidi ya Netanyahu na Gallant kwa kufanya jinai ikiwemo kutumia njaa kama silaha na kuwalenga raia ni ya haki.
Amefafanua kwa kusema: "ikiwa dunia haitazingatia sheria za kimataifa, tutaingia kwenye ushenzi zaidi. Nakubaliana na maamuzi ya ICC."
Netanyahu na wahalifu wengine wasiingie Marekani
Mji mmoja nchini Marekani umeahidi kumkamata Netanyahu na Gallant iwapo watakanyaga mji huo baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, kutoa vibali vya kuwakamata kutokana na jinai zao za kivita na na mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza.
Abdullah Hammoud, meya wa Dearborn katika jimbo la Michigan, amesema kwamba viongozi wa eneo hilo "watamkamata Netanyahu na Gallant ikiwa wataingia ndani ya mipaka ya jiji la Dearborn," akitoa wito kwa miji mingine ya Marekani kuiga mfano huo.
Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa X ameandika: "Miji mingine inapaswa kutangaza vivyo hivyo. Rais wetu anaweza asichukue hatua, lakini viongozi wa jiji wanaweza kuhakikisha Netanyahu na wahalifu wengine wa kivita hawakaribishwi kusafiri kwa uhuru kote Marekani."
Matamshi hayo yalikuja baada ya mahakama ya ICC, yenye makao yake makuu mjini The Hague, kuamua kuwa kuna "sababu za kuridhisha" za kuamini kuwa Netanyahu na Gallant wanabeba dhima kama washiriki wa "uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama mbinu ya vita; na uhalifu dhidi ya ubinadamu wa mauaji, mateso, na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu”.
Katika taarifa yake, jopo la majaji watatu wa ICC, limesema limekataa pingamizi la Israel dhidi ya mamlaka ya mahakama hiyo na kutoa vibali dhidi maafisa wa utawala huo.
Israel ilianzisha mashambulizi yake ya mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, baada ya kundi la muqawama la Hamas kutekeleza oparesheni yake ya kihistoria dhidi ya utawala huo ghasibu kwa lengo la kulipiza kisasi jinai zinazozidi kufanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.
Utawala wa haramu wa Israel hadi sasa umewaua Wapalestina wasiopungua 44,056, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine 104,268, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.
4249823