IQNA

Jinai za Israel

Israel imeua Wapalestina zaidi ya 100 huko Gaza baada ya mapatano ya usitishaji vita

22:51 - January 17, 2025
Habari ID: 3480064
IQNA-Idara ya Ulinzi wa Raia ya Gaza imetangaza leo Ijumaa kuwa Wapalestina wasiopungua 101, wakiwemo watoto 27 na wanawake 31, wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel tangu kutangazwa makubaliano ya kusitisha mapigano juzi Jumatano.

Wapalestina wengine 264 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Israel. Utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulizi hayo wakati hakuna ishara zozote wa kupungua hujuma za Israel dhidi ya Gaza. 

Huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, watu tisa wa familia ya mwandishi habari wa Kipalestina wameuliwa shahidi wakiwemo wanawake na watoto wadogo. 

Aidha Wapalestina wengine wawili wameuawa shahidi katika shambulio la anga la Israel katika eneo la al Balad katika mji wa Jabalia kaskazini mwa Gaza. 

Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimeushambulia vikali mji wa Jabalia tangu kutangazwa usitishaji vita Gaza juzi Jumatano. Watu wasiopungua 20 waliuawa katika mji wa Jabalia  katika mashambulizi ya anga ya Israel jana Alhamisi.

Eneo la mashariki mwa mji wa Khan Yunis pia halikusalimika na hujuma za kikatili za Israel, ambapo raia watano wameuawa katika shambulio lililolenga nyumba ya makazi ya raia.

3491487

captcha