IQNA

Kampeni ya ‘Kwa Jina la Ushindi’ ya kuhifadhi Surah Al-Fath

21:33 - February 18, 2025
Habari ID: 3480238
IQNA – Kampeni iliyopewa jina “Kwa Jina la Ushindi” imezinduliwa na Taasisi ya Astan Quds Razavi (Idara ya Mfawidhi wa Haram Tukufu ya Imam Ridha -AS-) nchini na itaendelea hadi mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa Hujjatul-Islam Seyed Masoud Mirian, mkurugenzi wa Kituo cha Masuala ya Qur’ani cha Taasisi ya Astan Quds Razavi, kampeni hii inalenga kuhifadhi Surah Al-Fath, sura ya 48 katika Qur’ani.

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika Makumbusho na Maktaba ya Kitaifa ya Malek, Tehran, Mirian alisema kuwa Surah Al-Fath ni miongoni mwa sura zinazotia moyo, kutuliza nafsi, na kuleta matumaini. Sura hii inapendekezwa kwa Waislamu ili kuwasaidia kuvuka changamoto ngumu zinazotokana na vita na vikwazo.

Alieleza kuwa wakati sura hii ilipoteremshwa, Waislamu walifikia hatua mpya katika harakati zao za kuunda jamii ya Kiislamu yenye mshikamano. Walijizatiti kwa pamoja ili kufanikisha ahadi zilizotolewa ndani ya sura hii.

“Tangu mwanzo wa Surah hii, waumini wanahakikishiwa utulivu wa ndani, na hivyo yeyote asiye muumini hataweza kupata amani ya kweli.”

Hujjatul Islam Mirian alisisitiza kuwa Surah Al-Fath inathibitisha ushindi wa hakika wa Upande wa Haki dhidi ya Upande wa Kufr.

Katika wakati ambapo kambi ya Muqawama au Mapambano ya Kiisalmu inakabiliana na kambi ya ubeberu wa dunia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashauri waumini kusoma Surah Al-Fath mara kwa mara.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo, Kituo cha Masuala ya Qur’ani cha Astan Quds Razavi kimeamua kuchukua hatua kwa vitendo.

“Kwa kuzingatia kuwa tunakaribia msimu wa kuchipua kwa Qur’ani na msimu wa kuchipua mazingira, na kwamba siku nyingi za Nowruz (mwaka mpya wa Kiirani)  zinasadifiana na siku za Ramadhani, tumezindua kampeni hii ya kuhifadhi sura teule za Qur’ani. Kutokana na umuhimu wake mkubwa, Surah Al-Fath ilichaguliwa kwa lengo hili.”

Aliongeza kuwa sikukuu za Nowruz (zitakazoanza Machi 21) ni fursa adhimu kwa wafanyaziara kutembelea mji mtakatifu wa Mashhad.

Kwa mamilioni ya wafanyaziara wanaosafiri kwenda Mashhad, kampeni hii, ambayo ni sehemu ya harakati ya kitaifa “Kuishi na Aya”, inalenga kuleta mshikamano zaidi kati ya harakati hii na kampeni ya Qur’ani, kwa lengo la kuwaweka watu karibu zaidi na Qur’ani.

3491906

Habari zinazohusiana
captcha