Katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, Imam Khamenei alikutana na wanazuoni na wasomaji mashuhuri wa kimataifa wa Qur’ani Tukufu wakati wa 'Mahafali ya Kushikamana na Kujikurubisha na Qur’ani.' Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Husainiya ya Imam Khomeini jijini Tehran mnamo Machi 2, 2025.
Wakati wa mkutano huo, Imam Khamenei alisisitiza hitajio la mtu binafsi na jamii kwa mafundisho ya tiba ya Qur’ani. "Jamii ya Qur’ani inapaswa kutenda kwa namna ambayo chemchemi za kiroho za Kitabu cha Mungu zinaingia ndani ya mioyo, akili, na hatimaye katika tabia na vitendo vya watu wote," alisema.
Baada ya kusikiliza kwa zaidi ya masaa mawili na nusu usomaji wa wasomaji au maqari wa Qur’ani pamoja na qasida za makundi ya Iran na kigeni, Imam Khamenei aliwapongeza hadhirina kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, akiutaja kuwa ni Idi kubwa na ya kweli kwa waumini. Alimhimidi Mwenyezi Mungu kutokana na ongezeko la wasomaji Qur’ani nchini, akiongeza kuwa hitaji la jamii kwa marejeo yasiyo na kikomo ya Qur’ani katika kushughulikia matatizo mbalimbali ni la kweli na la muhimu.
Katika kuelezea mahitaji ya mtu binafsi kwa Qur’ani Tukufu, alisema: "Tiba ya magonjwa yote ya kiroho na kimaadili ya binadamu - kama vile wivu, ubinafsi, kukata tamaa, uvivu, uroho, anasa, na kipaumbele cha maslahi binafsi juu ya manufaa kwa wote - inapatikana ndani ya Qur’ani."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kwa upande wa mahusiano ya ndani ya jamii, tunapaswa kuzingatia Qur’ani ili iweze kushughulikia masuala ya kijamii, ikiwa ni pamoja na haki ya kijamii, ambayo ni jambo la pili kwa umuhimu katika Uislamu baada ya Tawhid [umoja wa Mungu].
Imam Khamenei ameielezea Qur’ani Tukufu kama mwongozo wazi na sahihi katika uwanja wa mahusiano ya kimataifa, akieleza kuwa taifa la Iran halina matatizo na mataifa mengine. Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa sasa linakabiliana na mrengo mkubwa wa madola ya kiistikbari na kikafiri au ya kinafiki. Imam Khamenei amesisitiza kuwa Qur’ani Tukufu inatoa muongozo jinsi ya kushughulika na madola kama hayo katika hatua mbalimbali, ikionyesha wakati wa kuwasiliana, wakati wa kushirikiana, wakati wa kujibu kwa nguvu, na wakati wa kuchukua silaha.
Imam Khamenei amebaini kuwa usomaji sahihi na uskilizaji wa makini wa Qur’ani unaweza kusaidia kupunguza magonjwa yote ya binadamu, akiongeza kuwa wakati Qur’ani inaposomwa na kusikilizwa vizuri, inachochea hisia ya motisha kwa ajili ya kufuata haki na wokovu ndani ya mtu binafsi.
Akinukuu aya kutoka Qur’ani Tukufu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alibainisha kuwa kusudi la usomaji wa Mtume Muhammad (SAW) wa aya za Qur’ani ni pamoja na: utakaso; na hilo linatokana na kuwa Qur’ani ni tiba ya magonjwa yote ya kiroho na kihemko na ufundishaji wa Qur’ani. Ufundishaji hapa una maana ya elimu ya mfumo wa jumla wa maisha ya mtu binafsi na jamii; na kufundisha hekima, ambayo inahusu kutoa maarifa kuhusu ukweli wa ulimwengu. Aliendelea kusema kuwa usomaji Qur’ani ni jukumu ambalo alikuwa nalo Mtume (SAW), na kwamba wasomaji kimsingi wanatekeleza kazi ya Mtume (SAW).
Alibainisha kuwa moja ya kazi muhimu ya usomaji sahihi ni kubadilisha fikra za Qur’ani kuwa mawazo yanayokubalika kwa upana, akisisitiza athari ya Qur’ani kupitia usomaji wake kwa njia ya Tarteel. Katika kuelezea maana sahihi ya Tarteel, alifafanua kuwa Tarteel ni jambo la kiroho, ambalo linajumuisha usomaji kwa ufahamu na tafakari.
Imam Khamenei alielezea umuhimu wa kuelewa maana wakati wa usomaji, akisema: "Leo, kulinganisha na siku za mwanzo za Mapinduzi, wasomaji wetu wana ufahamu mzuri wa maneneo ya Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, ufahamu wa maana ya aya lazima upanuliwe kwa umma kwa ujumla."
Akiashiria ustawi mzuri wa sekta ya Qur’ani Tukufu nchini Iran, Imam Khamenei aliongeza: "Kwa bahati nzuri, nchi imepiga hatua za haraka katika uwanja wa Qur’ani. Tofauti na kipindi kabla ya Mapinduzi, wakati Qur’ani ilipuuzwa na usomaji wake ulifuatiliwa na watu wachache, leo tuna wasomaji wengi wenye vipaji na maarufu kote nchini, hata katika miji midogo na baadhi ya vijiji."
Imam Khamenei alielezea matumaini kuwa kwa kuzingatia nukta hizi muhimu, kiini cha kiroho cha Qur’ani kitaingia mioyoni, akili, na katika vitendo vya watu.
Chanzo: Khamenei.ir
3492126