IQNA

Ayatullah Khamenei: Hija ina manufaa kwa wanadamu wote

21:29 - May 04, 2025
Habari ID: 3480637
IQNA--Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, amesema kuwa lengo la Mwenyezi Mungu katika kwa kuweka ibada ya Hija ni kuwasilisha kielelezo kamili na kinachoelekeza namna ya kuendesha maisha ya binadamu, na akaongeza: muundo na sura ya dhahiri ya ibada hii ni ya kisiasa kabisa, huku maudhui yake yakiwa ya kiroho na ya ibada, ili kuhakikisha manufaa kwa wanadamu wote.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Ofisi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, siku ya Jumapili jijini Tehran alipokutana na waandaaji wa ibada ya Hija na kundi la wanaoelekea katika Nyumba Tukufu ya Allah, amesema: leo hii, faida kubwa zaidi kwa Umma wa Kiislamu ni umoja na mshikamano katika kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu, na lau kungekuwa na umoja huo, maafa kama ya Gaza na Yemen yasingetokea.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maarifa na ufahamu wa malengo na vipengele mbalimbali vya Hija kwa mahujaji ni utangulizi muhimu wa utekelezaji sahihi wa ibada hii adhimu, na kwa kurejelea aya nyingi za Qur’ani Tukufu, akaongeza: matumizi ya neno “nas” (watu) katika aya nyingi zinazohusu Hija yanaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu ameweka ibada hii kwa ajili ya kuongoza mambo ya wanadamu wote  na si Waislamu pekee; hivyo, kuendesha Hija kwa usahihi ni huduma kwa binadamu wote.

Katika kubainisha vipengele vya maarifa ya Hija aliitaja ibada hiyo kuwa ni ibada pekee ambayo muundo wake ni wa kisiasa kwa asilimia mia moja, kwa kuwa kila mwaka inawakusanya watu katika wakati na mahali pamoja kwa malengo maalumu, jambo ambalo kiasili lina upeo wa kisiasa.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: sambamba na muundo huo wa kisiasa, maudhui ya vipengele vya Hija ni ya kiroho na ya kiibada kwa asilimia mia moja, na kila kipengele kina ishara ya mfano na mafundisho kwa masuala na mahitaji mbalimbali ya maisha ya binadamu.

Katika kubainisha ishara hizo, alieleza somo la tawaf kama umuhimu wa kuzunguka kwenye mhimili na kituo cha tauhidi, na akaongeza: tawaf inamfundisha mwanadamu kuwa serikali, maisha, uchumi, familia na masuala yote ya maisha lazima yajengeke juu ya Tauhidi; kwa kufanya hivyo, mateso, mauaji ya watoto, na tamaa za kupindukia havitakuwepo, na dunia itakuwa bustani ya amani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akirejelea aya ya Qur’ani Tukufu, alieleza kuwa lengo la mkusanyiko wa Hija ni kuelewa na kufikia manufaa ya aina mbalimbali ya kibinadamu, na akasema: leo hii hakuna faida iliyo kuu kuliko umoja kwa Umma wa Kiislamu, na kwa kuwepo kwa umoja, mshikamano na kuunganika kwa Umma, matukio mabaya kama yanayoendelea Gaza na Palestina yasingetokea, na Yemen isingekuwa chini ya mashinikizo kama ilivyo sasa.

Akaeleza kuwa mgawanyiko na tofauti ndani ya Umma wa Kiislamu kunatoa fursa kwa madola ya kikoloni, Marekani, utawala wa Kizayuni na wenye tamaa kupitisha maslahi yao na malengo yao kwa mataifa, na akaongeza: kwa umoja wa Umma, usalama, maendeleo na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu pamoja na kusaidiana kati yao vinawezekana, na fursa ya Hija inapaswa kuangaliwa kwa mtazamo huo.

Ayatullah Khamenei amesisitiza nafasi na jukumu kubwa la serikali za Kiislamu, hususan nchi mwenyeji, katika kubainisha ukweli na malengo ya Hija, na akasema: viongozi wa nchi, maulamaa na wasomi, waandishi na watu wenye ushawishi kwa fikra za umma wana wajibu wa kuwabainishia watu ukweli wa Hija.

Habari zinazohusiana
captcha