Hujjatul Islam Mojtaba Heidari, mhadhiri katika Kituo cha Utafiti cha Hija na Ziyara za Kidini, ametoa tamko hilo katika mahojiano na IQNA.
Amesema kuwa baada ya kutekeleza ibada ya Hija na kurudi katika nchi zao, Waislamu huwatizama Waislamu wengine kwa mtazamo chanya. “Hii hisia chanya mbali na kumfaidi mtu binafsi, inakuza umoja wa kijamii na kudumisha umoja huo kwa muda mrefu.”
Hija ni ibada inayofanywa kwa pamoja, ambapo Waislamu wote wanachukua jukumu, amesema.
"Ibada ya Hija ina lengo la kuondoa utofauti na upendeleo wa kibinafsi, na watu hufanya ibada kwa usawa kabisa."
Amezingatia moja ya vipengele muhimu vya kutekeleza ibada ya Hija kuwa ni kutembea katika njia ya Mwenyezi Mungu na jambo hili huleta waumini pamoja.
Alitaja matokeo ya ibada ya Hija kama kuondoa mgawanyiko na amesisitiza wakati wa Hija hakuna mtu aliye na hali ya juu kuliko mwingine.
"Moja ya sifa ya Hija ni kwamba husaidia kufuta tofauti. Kwa mfano hali ya kuwa wote sawa huhisika wakati wa Hija katika amali za Tawaf au Sa'i kati ya Safa na Marwah, wakati ambapo pia hufanywa kitendo kiitwacho Harwala."
Hujjatul Islam Heidari amengeza kuwa Sa'i kati ya Safa na Marwah wakati wa ibada za Hija humfanya mtu yeyote mwenye kiburi kuwa mnyenyekevu, na unyenyekevu huu unaashiria heshima na kujitolea mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kuhusu faida ya makundi mbalimbali ya watu kukusanyika wakati wa ibada za Hija, amesema kuwa Hija sio tu kukusanyika kwa umma wa watu bali ni fursa kwa wanasiasa, wataalamu, na watu wenye ushawishi kukutana, kubadilishana mawazo, kuchunguza masuala makubwa yanayokabili dunia ya Kiislamu, na kutoa suluhisho za kukabiliana na changamoto hizi. “Suluhisho hizi zimekusudiwa kuwanufaisha Umma wa Kiislamu wote, si taifa moja tu.”
Amengeza kuwa uwepo wa watu kama hawa ni wa manufaa sana kwa sababu mbali na kuimarisha umoja na mshikamano, inasaidia kutatua masuala mengi ndani ya jamii ya Waislamu na dunia nzima kwa ujumla.
Alipoulizwa jinsi dhana kama udugu wa Kiislamu na umoja wa Umma unavyojidhihirisha wakati wa Hija, Hujjatul Islam Heidari ameeleza kuwa udugu wa Kiislamu unadhihirika wazi katika Hija na kuongeza kuwa udugu na umoja huu wa Kiislamu lazima uimarishwe zaidi kupitia juhudi za serikali za Kiislamu.
3493012