IQNA

Mkuu wa ICRO asifu shughuli za Qur'ani za Taasisi ya Ibn Sina nchini Russia  

21:10 - May 16, 2025
Habari ID: 3480693
IQNA – Mkuu wa Shirika la Iran la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu amepongeza juhudi za utafiti wa Quran zinazofanywa na Taasisi ya Ibn Sina nchini Russia.

 Katika ziara yake kwenye taasisi hiyo Jumatano, Hujjatul Islam Mohammad Mehdi Imanipour alisisitiza kuwa shughuli za masomo ya Qur'ani na sasisho la tovuti ya ‘Al-Quran’ kwa lugha ya Kirusi ni hatua muhimu na yenye matokeo katika kutekeleza maagizo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Wakati wa ziara hiyo, alizungumza na wakuu wa idara mbalimbali za taasisi hiyo na kupokea taarifa kuhusu shughuli za mwaka uliopita pamoja na mikakati itakayotekelezwa mwaka huu.

Hujjatul Islam Imanipour alisifu miradi mingi ya taasisi hiyo, ikiwemo historia ya simulizi, uhifadhi wa nyaraka, tafsiri na uchapishaji wa vitabu, pamoja na uandaaji wa matukio, hususan ushirikiano na wasomi na watafiti wa Kirusi.

Alisisitiza kuwa kazi maalum katika nyanja zote zina umuhimu mkubwa kwa hadhira, akiongeza kuwa uwepo wa taasisi hiyo katika majukwaa ya kisasa na anga ya kidijitali kwa lugha ya Kirusi, hususan katika masomo ya Qur'ani, ni jambo la msingi na maendeleo yake yatasaidia kuimarisha hadhi ya tafiti za Quran nchini Russia.

Hamid Hadavi, rais wa taasisi hiyo, alishukuru wazo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo lililopendekezwa na ICRO, pamoja na msaada wa shirika hilo tangu awamu za mwanzo za uanzishwaji wake.

Alielezea shughuli maalum zinazofanywa na ushirikiano na taasisi za Kirusi, watu mashuhuri na wanafikra kwa miaka iliyopita, ushiriki wa taasisi hiyo katika matukio mbalimbali ya kitamaduni nchini Russia kama maonyesho ya vitabu na uwasilishaji wa machapisho ya Sadra, pamoja na ushirikiano wa kitaaluma na vyuo vikuu, vituo vya kisayansi, na taasisi za elimu na utafiti za Iran na Russia.

Hadavi aligusia kuhusu kozi za mafunzo zinazofanywa na taasisi hiyo, akisema kuwa kwa kushirikiana na walimu wa Kirusi na Irani, taasisi inaratibu kozi maalum katika maeneo husika ambazo zimepata mapokeo mazuri na kuthaminiwa sana na hadhira ya Kirusi.

Taasisi ya Ibn Sina imekuwa ikifanya kazi ndani ya Shirikisho la Russiai tangu 2007 na ilianzishwa na Hujjatul Islam Imanipour, ambaye wakati huo alikuwa Mwambata wa Kitamaduni wa Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Moscow.

Taasisi hii inalenga kueneza elimu ya Uislamu kwa kuzalisha maudhui ya kisayansi na kitamaduni, kufanya tafiti za kielimu, kuandaa mikutano, kufundisha, kutafsiri, kuhariri na kuchapisha maandiko katika uwanja wa Uislamu na Waislamu kwa lugha ya Kirusi.

Hujjatul Islam Imanipour ameenda Urusi kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa utamaduni wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), uliofanyika Alhamisi, sambamba na Jukwaa la Kazan la Ulimwengu wa Kiislamu.

Kazan, mji mkuu wa Jamhuri ya Tatarstan ya Shirikisho la Russia, umechaguliwa kuwa Mji Mkuu wa Kitamaduni wa Kiislamu kwa mwaka wa 2025.

 3493101

captcha