IQNA

Israel yalaaniwa vikali kwa kuuhujumu Msikiti wa Al-Aqsa

10:27 - May 27, 2025
Habari ID: 3480745
IQNA – Zaidi ya walowezi 1,000 wa Kizayuni wa utawala haramu wa Israel wakiwa na mawaziri wa mrengo mkali wa kulia na wakisaidiwa na jeshi la utawala huo katili, wameuvamia Msikiti wa Al-Aqsa katika mji unaokaliwa wa al-Quds siku ya Jumatatu.

Uvamizi huo, ambao Wapalestina wanauona kama uchokozi wa makusudi, ulikuwa sehemu ya Maandamano ya Mwaka ya Bendera yanayoadhimisha uvamizi wa Israeli wa mwaka 1967 wa mji huo.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Palestina, WAFA, kundi hilo la walowezi lilijumuisha waziri wa Kizayuni mwenye misimamo mikali, Itamar Ben-Gvir, pamoja na mkewe na maafisa wengine wa Kizayuni. Tukio hilo liliendeshwa chini ya uangalizi wa jeshi la Israeli, ambalo kwa mujibu wa ripoti, liliwaruhusu kuingia katika eneo hilo kupitia Lango la Wamoroko.

WAFA, ikinukuu vyanzo vya ndani, ilisema kuwa takriban walowezi 1,500 waliingia katika viwanja vya Al-Aqsa na kufanya ibada za Kitalmudi, ambazo zinaonekana kuwa haramu na za kichokozi.

Zayuni mmoja anaripotiwa kupandisha bendera ya utawala haramu wa Israel na kucheza densi katika sehemu ya mashariki ya uwanja wa Msikiti, kitendo kilicholaaniwa vikali na maafisa wa Palestina waliokielezea kama uchochezi mkubwa. Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha walowezi wengine wakishiriki katika ibada za Kiyahudi ndani ya eneo hilo takatifu.

Mashuhuda waliiambia WAFA kwamba walowezi kadhaa walijaribu kuingiza kwa siri maandiko ya Taurati ndani ya eneo la Msikiti. Mikusanyiko mingine pia ilifanyika katika uwanja wa Ukuta wa Magharibi na karibu na Bab al-Qattanin, ambako washiriki walifanya maombi na kucheza.

Mvutano uliongezeka zaidi baada ya vikosi jeshi katili la Israel kuripotiwa kuwashambulia na kuwatoa kwa nguvu walinzi kadhaa wa Msikiti wa Al Aqsa. WAFA iliripoti kuwa zaidi ya maafisa wa Israel 200 walitumwa katika eneo hilo kuhakikisha walowezi wanapata fursa ya kuingia.

Kwingineko katika Mji wa Kale, walowezi wa Kizayuni  walitembea kupitia mitaa myembamba wakipeperusha bendera za utawala dhalimu wa Isarel wakigonga milango biashara zinazomilikiwa na Wapalestina ambazo zilikuwa zimefungwa, huku wakipiga nara za chuki dhidi ya Waarabu, zikiwemo “Kifo kwa Waarabu” na “Kijiji chenu na kiteketee,” kwa mujibu wa video zilizoshirikiwa na Mtandao wa Habari wa Quds.

Khatibu na Imamu wa Masjid al-Aqswa amelaani vikali vitendo hivyo vya kichokozi vya Wazayuni vyakulivunjia heshima eneo hilo takatifu na kueleza kuwa, vitendo hivyo vinavyojeruhi hisia za Waislamu viko wazi sasa kwa kila mtu.

Msikiti wa Al-Aqsa, ulioko Mashariki mwa al-Quds, unaheshimiwa kama sehemu ya tatu takatifu zaidi katika Uislamu baada ya Maka na Madina. Tangu uvamizi wa Israel wa mji huo katika vita vya mwaka 1967, eneo hilo limeendelea kuwa kitovu cha mvutano wa kidini na kisiasa. Ingawa ziara za wasiokuwa Waislamu zinaruhusiwa chini ya makubaliano ya hali ya sasa (status quo), sala za wasiokuwa Waislamu zimepigwa marufuku rasmi , sheria ambayo wachunguzi wanasema inavunjwa kwa kuungwa mkono kwa kificho na mamlaka za Israel.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas,  imelaani uvamizi huo wa walowezi na kuutaja kuwa ni “ukiukwaji wa wazi wa utakatifu na hadhi ya Msikiti wa Al-Aqsa.” Hamas imeahidi kwamba Wapalestina wataendelea kulilinda eneo hilo takatifu na kupinga kwa nguvu yoyote juhudi za kuligawanya au kuligeuza kuwa ya Kiyahudi.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeonya kuwa uvamizi huo ulikuwa ni “uenezaji taharuki kwa makusudi” na matusi ya moja kwa moja kwa hisia za kidini za Waislamu duniani kote. OIC imesisitiza kuwa Msikiti wa Al-Aqsa “kwa ukamilifu wake” ni wa ibada ya Waislamu pekee na kuitaka jumuiya ya kimataifa kusitisha ukiukaji unaojirudia wa utakatifu wa eneo hilo.

3493240

 

captcha