IQNA

Kadhia ya Al Aqsa

Wapalestina wahimizwa kuandamana kwenye Msikiti wa Al-Aqsa Ramadhani Mosi

17:22 - February 29, 2024
Habari ID: 3478432
IQNA-Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amewataka Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu Israel kuandamana hadi Msikiti wa Al-Aqsa katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ismail Haniyah amesema katika ujumbe wa televisheni kwamba: "Kuzingirwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa na kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza ni kitu kimoja." 

Haniyeh alikuwa akijibu tangazo lililotolewa na utawala wa Israel kwamba utaweka vizuizi vya kuingia Msikiti wa Al-Aqsa katika Mji Mkongwe wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu wakati wa mfungo wa Ramadhani eti kulingana na "mahitaji ya usalama."

Siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu inasadifiana na Machi 11 au 12.

Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Hamas amesema: "Msikiti wa Al-Aqsa na maeneo mengine matakatifu lazima yasimamiwe kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Watu wetu watatetea misikiti, makanisa, na maeneo yao matakatifu kwa kila aina ya mapambano."

Ismail Haniyah amesema, kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni sehemu ya mpango wa kuwafurusha Wapalestina wote katika ardhi na nchi yao.

Kihistoria, mwezi wa Ramadhani umekuwa ukishuhudia ongezeko la hujuma na mashambulizi ya Israeli dhidi ya Wapalestina, haswa karibu na Msikiti wa Al-Aqsa.

Ramadhani ya mwaka huu inatazamiwa kuwa na vurugu zaidi kuliko miaka iliyopita kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanwya na utawala katili wa Israel dhidii ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Sambamba na mauaji ya raia elfu 30 wa gaza, utawala wa kigaidi wa Israel unaosaidiwa na Marekani pia umeua Wapalestina karibu 500 wa ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tangu baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa, tarehe 7 Oktoba mwaka jana. 

3487371

Kishikizo: al aqsa ukanda wa gaza
captcha