Harakati ya Kiislamu ya ukombozi wa Palestina, Hamas, imelaani uvamizi huo na kuutaja kuwa"msukosuko hatari" na ukiukwaji wa haki za Wapalestina. Uvamizi huo, uliofanywa pamoja na makazi ya Israel, ulitokea Jumatano huku vita vya mauaji ya kimbari vya Israel vikiendelea huko Gaza.
Kwenye tamko lao, Hamas ilieleza uvamizi huo kuwa sehemu ya juhudi za utawala ghasibu wa Israel kubadilisha utamabulisho wa eneo hilo takatifu. Kikundi hicho kiliitaka kuongezeka kwa uamsho wa Wapalestina dhidi ya majeshi ya Israel kukabiliana na "ukiukaji wa kimfumo" wa Al-Aqsa.
Tamko hilo liliitaka Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuchukua hatua za moja kwa moja kukabiliana na vitendo vya Israel katika eneo hilo, huku likionya kwamba uvamizi kama huo unaweza kuzidisha mvutano zaidi.
Hii ni mara ya sita Ben-Gvir kuvamia uwanja wa Al-Aqsa tangu ajiunge na baraza la mawaziri la Netanyahu mwaka 2022.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia pia imelaani uvamizi huo. Vile vile, Wizara ya Mambo ya Nje ya Egypt imeonya kwamba hatua hiyo inaweza kuchochea mvutano zaidi katika maeneo yaliyovamiwa ya Palestina, ikihatarisha utulivu wa eneo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan pia imekosoa vikali uvamizi huo kuwa "uchochezi wa makusudi," ikisisitiza kwamba Israel haina mamlaka juu ya Quds Mashariki iliyovamiwa wala maeneo yake ya Kiislamu na Kikristo.
Turkey pia imekosoa uchochezi huo. "Hatua hii ya wafuasi wa (waziri mkuu wa Israel, Benjamin) Netanyahu ni uamuzi hatari ambao utazidisha mvutano tena katika mkoa," ilisema tamko la Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.
Idara ya Wakfu wa Kiislamu katika mji wa Quds nayo imetoa taarifa ya kulaani kitendo hicho cha uchochezi kilichofanywa na Ben Gvir.
Huko nyuma pia, waziri huyo wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni alishawahi mara kadhaa kuwatolea mwito Wazayuni wauvamie Msikiti wa Al-Aqsa.
Kitambo nyuma, Ben Gvir aliandamana na mamia ya walowezi wa Kizayuni na kufanya kitendo cha kichochezi cha kuuvamia Msikiti wa Al-Aqsa. Waziri huyu mwenye misimamo mikali ya chuki alidai: "sera yetu inaturuhusu kusali kwenye Mlima wa Hekalu (Msikiti wa Al-Aqsa). Sheria huko iko sawa kwa Wayahudi na Waislamu, na ninapanga kujenga sinagogi huko".
Waziri huyo mlowezi wa Kizayuni amechukua tena hatua ya kuuvunjia heshima Msikiti wa Al-Aqsa katika hali ambayo, tangu utawala ghasibu wa Israel ulipoanzisha vita vya kinyama na jinai dhidi ya Ukanda wa Gaza Oktoba 2023 hadi sasa umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 50,000.
Katika kipindi hiki, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu nazo pia zimekuwa uwanja wa mapigano kati ya askari wa Kizayuni na Wapalestina wenye hasira na kupelekea kuuawa shahidi mamia ya Wapalestina.
3492554