Falsafa muhimu zaidi ya Hija ni mabadiliko ya maadili. Ibada ya Ihram humsaidia anayehiji kutoka katika sura za mafungamano ya kidunia. Kwa kupigwa marufuku kwa starehe za dunia na kuzingatia kujiboresha kiroho, wakati anayehiji anapokuwa Muhrim, yaani yaliyevaa vazi maalumu la Ihram, anajitenga na ulimwengu wa kimaada na kuingia katika ulimwengu wa kiroho na utulivu.
Kisha anatekeleza amali zote za ibada ya Hija moja baada ya nyingine, ambayo kila moja ina maana ya kina ya uhusiano wake wa kiroho na Mwenyezi Mungu, inamsaidia kumkaribia Mwenyezi Mungu, inamuweka mbali na maisha yake ya nyuma ya giza na madhambi, na inamleta karibu na mustakbali mzuri uliojaa nuru na utulivu.
Mapinduzi haya ya kimaadili yanazidishwa kwa kuzingatia ukweli kwamba taratibu hizi katika kila hatua ni ukumbusho wa juhudi na dhabihu zilizofanywa na Nabii Ibrahim (AS) ambaye ni maarufu kama mvunja masanabi, mwanawe Ismail (AS) na mkewe Hagar, na ukweli kwamba ardhi ya Makka kwa ujumla na hasa Msikiti Mkuu ni ukumbusho wa yale yaliyomtokea Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na Waislamu katika miaka ya mwanzo baada ya kuja kwa Uislamu.
Katika kila pembe ya Msikiti Mkuu na ardhi ya Makka, waumini huhisi uwepo Mtukufu Mtume Muhammad (SAW), Imam Ali (AS) na viongozi wengine wa kidini.
Haya yote yanaweka misingi ya mapinduzi ya kimaadili katika nyoyo zilizo tayari kwa ajili yake, kugeuza ukurasa wa maisha kwa njia isiyoelezeka na kufungua ukurasa mpya katika maisha ya Mahujaji.
Ndio maana tunasoma katika Hadithi kwamba mwenye kuhiji anarudi kabisa kutoka Hija akiwa msafi na asiye na madhambi kama siku ambayo mama yake alimzaa.
Hija ni kuzaliwa mara ya pili kwa Waislamu na mwanzo wa maisha mapya ya mwanadamu. Bila shaka baraka kama hiyo ni kwa wale ambao wamefikia mwisho wa mafundisho na roho ya Hija.
3488681