IQNA

Uzinduzi wa Wiki ya Kimataifa ya Maadhimisho ya Idi ya Ghadir

15:29 - June 11, 2025
Habari ID: 3480824
IQNA – Idara ya Mfawidhi wa Haram Takatifu ya Imam Ali (AS), imtangaza kuanza kwa maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Idul Ghadir, yakihusisha ushiriki kutoka zaidi ya mataifa 40 katika mabara matano.

Sheikh Haidar Rahim, mkuu wa kitengo cha habar cha idara hiyo, amesema kuwa maadhimisho haya yatajumuisha shughuli na vipindi mbalimbali vya kijamii, kielimu, na kiutamaduni. Kilichoangaziwa zaidi ni ushiriki mpana, ambapo zaidi ya bendera 700 za Idul Ghadir zimepandishwa ndani ya Iraq na katika mataifa mengine duniani.

Ameeleza kuwa bendera ya Ghadir imepandishwa katika zaidi ya mataifa 40, ikiwemo nchi za Ulaya, majimbo matano ya Marekani, na pia bendera tatu ndani ya Iran, kwa mashirikiano na msaada wa Astan ya Haram ya Imam Ali (AS).

Kwa mujibu wa Rahim, shughuli hizi zitajumuisha makongamano ya kielimu, matamasha ya Qur’ani, mikusanyiko ya Ghadiriyah, pamoja na vipindi maalum kwa watoto na watumishi wa Haram Takatifu.

Zaidi ya hafla arobaini zimepangwa kufanyika katika wiki hii iliyoanza Jumatatu, tarehe 9 Juni, 2025. Miongoni mwa matukio hayo ni maandamano maalum ya watoto yatima, yakihusisha zaidi ya watoto elfu moja kutoka mji mtukufu wa Najaf, ambao watafanya bay’ah (kiapo cha utii) kwa Imam Ali (AS).

Rahim aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza, tamthilia kubwa ya kisanii kuhusu tukio la Ghadir itaoneshwa katika mkoa wa Najaf. Tamthilia hiyo itafanyika kwenye uwanja wenye ukubwa wa mita za mraba 10,000, na itaweza kuhudumia watazamaji zaidi ya 5,000, kwa muda wa wiki nzima.

Astan pia imeanza kuupamba mji wa Najaf, ambapo maeneo yenye mapambo yamefikia zaidi ya mita za mraba 35,000.

Tukio la Ghadir, linalofahamika kama Idul Ghadir, huadhimishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani kote kila mwaka. Ni miongoni mwa sikukuu tukufu na zenye furaha kwa Mashia, inayofanyika kila tarehe 18 ya Dhul Hijjah kwa mujibu wa kalenda ya Hijri ya mwezi, ambayo mwaka huu inasadifiana na Jumamosi, tarehe 14 Juni.

Ni siku ambayo, kwa mujibu wa riwaya zilizothibiti, Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) alimteua Imam Ali bin Abi Talib (AS) kuwa Khalifa na kiongozi baada yake kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

3493402

captcha