IQNA

Waislamu leo wanaadhimisha kuzaliwa Imam Ali (AS)

13:40 - January 14, 2025
Habari ID: 3480053
IQNA--Leo tarehe 13 mwezi Rajab, ni siku ya kukumbuka kuzaliwa Amirul Muuminin, Imam Ali bin Abi Twalib (AS) ambapo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaadhimishwa pia kama Siku ya Baba.

Leo tarehe 13 Rajab zinaanza siku zinazojulikana katika dini kuwa ni "Siku Nyeupe" au siku za ibada ya Itikafu ambazo ni siku za tarehe 13, 14 na 15 za mwezi huu wa Rajab.

Katika siku hizi waumini wanashauriwa kufanya ibada ya itikafu ya kukaa na kubaki katika sehemu au mahali maalumu hususan misikitini na maeneo matakatifu kwa ajili ya ibada na kumdhukuru Mwenyezi Mungu SW. Watu wanaofanya itikafu hutakiwa kufunga Saumu siku tatu mfululizo wakiwa katika jitihada za kuondoka katika minyororo ya dunia hii finyu na kujikuribisha kwa Allah.

Ibada ya itikafu imehimizwa sana na Mtume Muhammad (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake.

Imam Ali bin Abi Twalib, Swahaba wa karibu zaidi kwa Mtume Muhammad (saw) na Imam wa kwanza wa Waislamu katika kizazi chake, alizaliwa  katika Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba. Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib.

Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.   

Siku ya kuzaliwa Imam Ali (AS) imepewa jina la Siku ya Baba, ili kutambua mchango wa baba katika familia na jamii, kujitolea kwa akina baba na majukumu yao kama nguzo za maisha ya familia, suala ambalo lina mizizi katika mafundisho ya Kiislamu na utamaduni wa Iran.

Katika utamaduni wa Kiislamu, jukumu la baba linatambuliwa kuwa msingi wa utulivu wa familia na jamii. Katika mila na utamaduni wa Iran pia, akina baba wanaheshimiwa kama nembo ya hekima, mamlaka na kujisabilia.

Siku ya Baba inasadifiana na kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali (AS), kielelezo cha kudumu cha uadilifu, upendo, na ubaba usio na kifani katika historia ya Kiislamu. Akijulikana kwa ushujaa na hekima yake, Imam Ali (AS) pia anaadhimishwa kwa nafasi yake kuu katika kutoa malezi kama baba. Historia inasimulia maingiliano yake ya upendo na watoto wake, ikimdhihirisha kama mfano wa ubaba wenye upendo na huruma.

Chaguo la kuoanisha Siku ya Taifa ya Baba na kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) linaonyesha muungano mkubwa wa maadili ya kidini na kitamaduni katika jamii ya Iran.

Nchini Iran, familia zinaadhimisha siku hii kwa watoto na akina mama kuwapa baba zao zawadi za aina mbalimbali zikiwemo kazi za kutengeneza kwa mikono, vitabu au mashada ya maua, na mara nyingi familia hukutana nyumbani kwa baba na kupata chakula kwa pamoja. 

3491451

Kishikizo: imam ali 13 rajab
captcha