IQNA

Iran yazindua mpango mkubwa wa kitaifa kuadhimisha Idul Ghadir

15:39 - June 11, 2025
Habari ID: 3480825
IQNA – Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Iran imepanga shughuli na maadhimisho ya kitaifa yenye sura ya kitamaduni, kidini na kijamii kwa ajili ya kusherehekea Sikuukuu ya Ghadir (Idul Ghadir), likiwa ni tukio mashuhuri linaloenziwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani kote.

Hii ilibainishwa Jumanne katika mkutano wa waandishi wa habari uliohutubiwa na Hujjatul-Islam Kamal Khodadadeh, Naibu wa Muda wa Sherehe na Masuala ya Mikoa katika Baraza la Kuratibu Uenezi wa Kiislamu.

Amesema: "Zaidi ya taasisi 50 za kitamaduni zinashiriki chini ya mwongozo wa baraza hili, kwa lengo la kueneza mafundisho ya Uislamu kupitia maadhimisho haya."
Mwaka huu, msisitizo umewekwa kwenye Nahj al-Balagha, mkusanyiko mashuhuri wa khutba na maneno ya hekima ya Amir al-Mu’minin Imam Ali (AS), ili kuongeza uelewa wa kina wa mafundisho yake.

Matembezi ya sherehe yenye urefu wa kilomita nyingi yatakuwa miongoni mwa shughuli kuu katika miji mbali mbali. Khodadadeh amesema kuwa hayo ni matukio ya barabarani yanayoweza kuwa majukwaa ya kiutamaduni ya muda mrefu, yakijumuisha michezo ya watoto na vibanda vya kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina.

Ametangaza kuwa tukio la kihistoria la Ghadir Khumm litawasilishwa kama tamthilia katika maeneo 149 kote nchini, kwa mtindo unaojumuisha vipengele vya kihistoria, kisanii na kielimu. Katika kampeni maalum iitwayo kwa jina la Imam Ali (AS), wafungwa 110 waliofungwa kwa makosa ya bahati mbaya watapewa msamaha katika kila jimbo.

Ugawaji wa chakula ni sehemu muhimu ya maadhimisho. Kupitia kampeni ya "Mitaa ya Alawi", wakazi wameshauriwa kupika chakula cha ziada na kushirikiana na majirani. Khodadadeh alisema kuwa kampeni hiyo haijahifadhiwa tu kwa siku ya maandamano bali pia inatekelezwa katika mitaa mbalimbali.

Mawkib au vibanda vya huduma za kidini  zaidi ya 2,400  vitawekwa kwenye njia kuu ya matembezi ya Sikukuu ya Ghadi mjini Tehran, kutoka Medani ya Azadi hadi Medani ya Imam Hossein. Khodadadeh amesema: "Tumejifunza mengi kutoka miaka iliyopita. Tumeweka mikakati na uratibu bora ili kuboresha tukio hili kila mwaka."

Akitaja utofauti wa mwaka huu, alieleza kuwa kutakuwa na vibanda maalum vinavyoangazia watoto, familia, utamaduni wa muqawama (mapambano ya haki) na mafundisho ya Nahj al-Balagha.

Khodadadeh alisisitiza kuwa Imam Ali (AS) ni kielelezo cha umoja kati ya Sunni na Shia, akifichua kuwa matembezi au maandamano haya ya furaha yatafanyika katika kila jimbo, ikiwemo yale yenye wakazi wengi wa Kisunni kama Kurdistan, Golestan na Hormozgan, ambako jamii za Kisunni zitaandaa matukio yao wenyewe.

Ametangaza pia kuwa kutakuwa na mkutano maalum wa Sayyid wa Kisunni huko mkoa wa Hormozgan. Katika uwanja wa kimataifa, programu maalum kuhusu Imam Ali (AS) zitafanyika katika zaidi ya vyuo vikuu 200 duniani, hasa miongoni mwa wanafunzi. Madarasa ya mtandaoni na makongamano ya kielimu juu ya Nahj al-Balagha na maisha ya Imam Ali (AS) pia yamepangwa.

Katika hatua ya ishara ya mapenzi kwa watu wa Ahlul Bayt (AS), maua 60,000 yametolewa na umoja wa wauzaji maua wa kitaifa wa Iran kwa ajili ya mapambo ya makaburi matukufu ya Imam Ali (AS), Imam Hussein (AS), na maeneo mengine ya ziara nchini Iraq.

Khodadadeh pia alisema kuwa vikundi vya maqari wa Qur'an watasoma Hotuba ya Ghadir katika Haram ya Imam Ali (AS) na maeneo mbalimbali duniani.

Tukio la Ghadir au Eid al-Ghadir huadhimishwa kila mwaka na Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia kote ulimwenguni kama moja ya sikukuu kubwa za furaha, likiwa ni kumbukumbu ya siku ambayo Mtume Muhammad (SAW) alimteua Imam Ali ibn Abi Talib (AS) kuwa Khalifa na Imam baada yake kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Mwaka huu, maadhimisho ya Eid al-Ghadir yatakuwa siku ya Jumamosi, tarehe 14 Juni, sambamba na tarehe 18 Dhul Hijjah kwa mujibu wa kalenda ya Hijri ya mwezi.

3493410

 

captcha