IQNA

Ayatullah Khamenei: Idul Ghadir ni sikukuu ya kipekee kwa Waislamu

13:43 - June 12, 2025
Habari ID: 3480826
IQNA – Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ametaja Idul-Ghadir, ambayo mwaka huu inaangukia tarehe 14 Juni, kuwa ni siku ya kipekee kwa Umma wa Kiislamu.

Katika kikao kilichofanyika Jumatano jijini Tehran, tarehe 11 Juni 2025, Imam Khamenei alikutana na Spika na wajumbe wa Bunge la 12 la Iran ambalo ni maarufu kama Majlis ya Ushauri ya Kiislamu.

Akiwakaribisha kwa salamu za kheri na fanaka kwa munasaba wa sikukuu ya Idul-Ghadir, Kiongozi "Kiongozi Muadhamu ameitaja Idi hiyo kuwa tukio muhimu kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu. Aidha amesema Idul Ghadir inaweza  kuchangia uelewa kina kuhusu dini ya Uislamu. Pia alitoa pongezi kwa hadhira kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Imam Hadi (AS).

Imam Khamenei amebainisha kuhusu hadhi ya mabunge duniani kuwa ni jambo linalotambulika kimataifa, akisema kuwa hadhi hiyo inatokana na uzito wa sheria zenyewe. “Sheria ni msingi wa kuwepo kwa maisha ya kijamii,” alisema, akiongeza kuwa kwa mujibu wa mantiki, sheria zinazotungwa na akili ya pamoja kupitia wawakilishi wa taifa huwa na uzito na uhalali mkubwa zaidi.

Kiongozi Muadhamu alibainisha tofauti iliyopo kati ya nafasi ya kisheria ya mabunge na uzito wa kweli wa kazi zao, akisema kuwa maadili na athari halisi ya mabunge hutofautiana sana. “Heshima ya kweli ya bunge lililoasisiwa juu ya misingi ya dini, lenye wanachama wacha Mungu, waaminifu, wanaosimama na haki, na kutetea wanyonge huku wakipinga dhulma, haiwezi kulinganishwa na bunge lililojaa watu wasiojali, linalochangia dhulma, ubaguzi, ukosefu wa usawa na hata kuunga mkono wauaji wa watu wa Gaza,” alisema.

Imam Khamenei alimpongeza Mheshimiwa Mohammad Bagher Ghalibaf kwa kuchaguliwa tena kama Spika wa Majlis, na kisha akatoa maelekezo kuhusu misingi ya kulinda heshima ya kweli ya bunge hilo. Aliwataka wabunge kuwa na uchaji wa Mwenyezi Mungu, kuwajibika mbele ya sheria, na kutanguliza radhi ya Allah na maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi.

Aidha, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa kauli za wabunge zina uzito mkubwa na zinapaswa kuhamasisha matumaini na kuleta utulivu nchini. Aliwakumbusha kuwa kauli zao ziwe na hekima, msimamo wa Mapinduzi ya Kiislamu, na uwepo wa azma thabiti ya kitaifa.

Akizungumzia sifa ya taifa la Iran, Imam Khamenei alilisifu taifa hilo kwa kusimama kidete dhidi ya vitisho na propaganda za madola makubwa. Alitaja ushiriki mkubwa wa wananchi katika kumbukumbu ya kufariki kwa Imam Khomeini na maandamano ya Bahman 22 kama ushahidi wa nguvu na ari ya wananchi. “Nguvu hii inapaswa kudhihirika katika misimamo ya wabunge, katika kupitisha au kupinga sheria na watu,” alisema, na kuongeza kuwa wabunge wa sasa wanaonyesha sifa hizi kwa kiwango kikubwa.

Alisisitiza umuhimu wa kuwa na mwelekeo wa kimapinduzi ndani ya Majlis kama nguzo ya kuendeleza hadhi yake ya kipekee. “Majlis ni bunge la kimapinduzi, lakini kuwa mwanamapinduzi haimaanishi kwa maneno makali tu. Kuweni waangalifu msije mkakosea maana ya kuwa mwanamapinduzi,” alionya.

Imam Khamenei amesema mwenendo wa kimapinduzi ni kushikamana na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu bila kuyumba, kuonyesha ujasiri, na kueleza imani kwa njia sahihi, isiyo ya matusi, wala kebehi, huku mkiepuka misukumo ya maslahi binafsi au vyama. “Dunia ipo mbele ya Mwenyezi Mungu, na kwa mtazamo huu tu ndio tunapaswa kutafuta radhi Zake. Lazima tuoneshe kwa uthabiti msimamo wa Mapinduzi na kuufuata katika maamuzi yetu,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wabunge kuwa na msimamo wa pamoja, imara na wa wazi dhidi ya mashambulizi ya kijinga ya wanaopinga Jamhuri ya Kiislamu ,akilielezea hilo kama jukumu jingine la mwenendo wa kimapinduzi.

Mwanzoni mwa kikao hicho, Spika Mohammad Bagher Ghalibaf alielezea mafanikio ya Bunge la 12, akitaja utekelezaji wa Sheria ya Hatua ya Kimkakati ya Kulinda Maslahi ya Taifa, pamoja na kuunga mkono nafasi ya heshima ya diplomasia ya nchi katika mazungumzo ya Muscat. Aliongeza kuwa “ushiriki hai wa wabunge katika diplomasia ya bunge,” “kupitishwa kwa Sheria ya Kodi ya Faida ya Mitaji,” “kuidhinishwa kwa muundo wa jumla wa Mpango wa Kitaifa wa Akili Mnemba,” “marekebisho ya sheria ya usimamizi wa bunge,” na “utekelezaji wa mifumo ya kidijitali katika bajeti na usimamizi wa fedha” ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Bunge hilo.

Chanzo: Khamenei.ir

captcha