IQNA

Maktaba ya Msikiti wa Mtume yatoa huduma kwa watafiti na wageni

21:47 - July 12, 2025
Habari ID: 3480932
IQNA – Maktaba ya Msikiti wa Mtume au Al Masjid An Nabawi mjini Madina inafanya kazi kama taasisi ya umma inayotoa huduma mbalimbali kwa watafiti na wageni wanaovutiwa na turathi za Kiislamu.

Kwa mujibu wa Sabq.org, maktaba hii ni miongoni mwa vituo vinavyoongoza kwa maarifa katika ulimwengu wa Kiislamu. Ikiunganisha hazina kubwa ya maandiko adimu na vitabu rejea pamoja na zana za kisasa za utafiti wa kidijitali, maktaba inalenga kuhifadhi urithi wa maandishi ya Kiislamu kupitia miundombinu ya kisasa.

Ilianzishwa mwaka 1933 (1352 Hijria) kufuatia pendekezo la Obaid Madani, aliyekuwa mkurugenzi wa wakfu wa Madina wakati huo. Hata hivyo, baadhi ya vitabu vilikuwa tayari vimehifadhiwa katika eneo la Rawdha Sharifah kabla ya tarehe rasmi ya kuanzishwa.

Maktaba ina kumbi tofauti za kusomea kwa wanaume, wanawake, na watoto; sehemu maalum ya maandiko adimu; maktaba ya sauti inayohifadhi mawaidha na khutuba zilizotolewa ndani ya Msikiti wa Mtume; na kitengo cha kiufundi kinachoshughulikia ukarabati wa vitabu.

Sehemu maalum ya vitabu adimu hujumuisha machapisho yaliyoteuliwa kwa kuzingatia historia ya kuchapishwa, mapambo, muundo wa kimwili, au michoro. Kitengo cha kidijitali kinawawezesha watumiaji kuvinjari orodha ya maktaba na kutembelea tovuti za Kiislamu, zikiwemo maktaba nyingine za kidijitali, kupitia kompyuta zilizounganishwa na Wi-Fi.

Mkusanyiko wa maktaba unajumuisha zaidi ya vitabu 182,000 katika fani 71 za kielimu kwa lugha 23. Pia kuna zaidi ya machapisho ya kidijitali 143,000 na kurasa milioni 43 za kidijitali. Kompyuta 70 zinapatikana kusaidia tafiti za kitaaluma.

Baadhi ya vitabu vya maktaba vilipotea katika moto uliotokea msikitini tarehe 13 Ramadhani mwaka 886 Hijria, lakini maandiko ya thamani kama vile misahafu ya maandishi ya mkono na nakala adimu bado yanapatikana.

Maktaba hii iko wazi saa 24 kila siku karibu na Lango la 10 upande wa magharibi wa msikiti, na inasimamiwa na Idara Kuu ya Masuala ya Misikiti Miwili Mitakatifu.

4293436

captcha