IQNA

Kuhifadhi Qur’ani kumeleta maana na utulivu maishani, asema Mama Muislamu wa Iran

15:30 - July 13, 2025
Habari ID: 3480938
IQNA – Zohreh Qorbani, mama mchanga kutoka Iran, asema kuwa kuhifadhi Qur’ani Tukufu kumemletea mpangilio, utulivu wa moyo, na uwazi wa kiroho katika maisha yake ya kila siku licha ya changamoto anazokumbana nazo.

Bi. Qorbani alianza safari yake na Qur’ani akiwa na umri mdogo, sambamba na dada yake. Kile kilichoanza kama shughuli ya kujifurahisha kwenye madarasa ya mtaani, baadaye kiligeuka kuwa ahadi ya kiroho iliyojaa mapenzi kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. “Mwanzoni ilikuwa kama burudani tu,” amekumbuka katika mazungumzo na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA), “lakini kushiriki kwa mara kwa mara kulipanda mbegu ya mapenzi ya Qur’ani moyoni mwangu.”

Alipofika umri wa miaka 12, Qorbani alirudi tena kwenye masomo ya usomaji na kuhifadhi Qur’ani. Hata hivyo, safari haikuwa nyoofu kwani kulikuwepo na vipingamizi kutokana na masomo ya kawaida na vishawishi vya ujana.

“Kila nilipojiondoa mbali na Qur’ani, nilihisi ombwe kubwa, hasa kihisia. Hisia hiyo ilinivutia tena kuelekea katika Qur’ani na kila mara niliporudi, nilikuwa na nia iliyo imara zaidi,” alieleza.

Anamkumbuka baba yake kama nguzo kuu ya kumtia moyo. “Hakufunza tu kuhusu Qur’ani bali aliishi nayo. Mtindo wake wa maisha ulitufundisha kimya kimya. Alituchukua kwa subira madarasani na alitusomesha pia. Sasa kwa kuwa mimi ni mama, natambua thamani ya juhudi zake kwa undani zaidi.”

Kwa sasa, Qorbani ameshahifadhi sehemu saba (Juzuu) za Qur’ani. Njia yake ni ya utulivu na imezingatia mazingira yake ya sasa. “Nikiwa na mtoto mdogo nyumbani, mara nyingi hurudia aya wakati nikiwa nafanya kazi za nyumbani au mapumziko mafupi. Huenda siendi kasi kama wengine, lakini ni endelevu na ina maana kubwa kwangu.”

Anataja kuhifadhi Qur’ani si tu ibada, bali pia ni nguvu thabiti ya maisha ya kila siku. “Kuna siku akili yangu huwa imevurugika au nahisi mzigo mwingi wa mawazo, lakini Qur’ani hunituliza. Huniweka sawa na imeathiri kwa njia chanya maamuzi yangu na mahusiano yangu. Qur’ani imenipa mwelekeo;  si katika kiroho tu, bali hata katika maisha yangu yote.”

Ingawa binti yake bado ni mdogo, Bi. Qorbani ameshaanza kumfundisha sura fupi fupi za Qur’ani. “Nadhani watoto hujifunza zaidi kutoka kwenye mazingira kuliko mafundisho ya moja kwa moja. Mama anaposoma Qur’ani mwenyewe, hali hiyo hujenga mazingira ya kiimani ndani ya nyumba. Wakati wa ujauzito wangu, nilihitimisha Qur'ani mara kadhaa, na naamini ndiyo maana binti yangu tayari anaonyesha hamu.”

Alipoulizwa namna ya kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kuhifadhi Qur’ani, Qorbani alisisitiza umuhimu wa kuionesha Qur’ani kama mwongozo hai wa maisha. “Vijana wa leo wanatafuta maana ya kina. Tukiwafundisha Qur’ani kama wajibu tu, tutawapoteza. Lakini tukionesha Qur’ani inavyohusiana na maisha yao halisi, mahusiano, changamoto, na mafanikio binafsi, basi watavutiwa. Qur’ani si tu jukumu; ni fursa ya kujenga maisha bora.”

Ujumbe wake kwa wanawake na wasichana wenye majukumu mengi ni rahisi: anza kidogo.
“Hata kama una dakika tano tu kwa siku, zitolee Qur’ani. Usisubiri uwe na wakati kamili, hauji kamwe. Anza na aya moja tu, utaona jinsi Qur’ani inavyoanza kujipa nafasi maishani mwako na kuibadilisha. Hakuna anayekuwa hafidh mara moja, lakini kila anayechukua hatua ya kwanza huongozwa na Mwenyezi Mungu.”

3493814

captcha