Profesa Saeed Nazari, ambaye anaongoza tawi la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia huko Hamedan, alisema mjumuiko mkubwa wa Arbaeen unaonyesha nguvu ya mrengo wa hakii na inatia hofu katika mioyo ya maadui wa Uislamu.
Sio tu Waislamu wa madhehebu ya Shia, lakini pia Masunni na hata wasio Waislamu wanashiriki katika mjumuiko huu wa kila mwaka nchini Iraq, alibainisha.
Hii inaashiria mapenzi kwa Imam Hussein (AS) miongoni mwa wafuasi wa madhehebu na dini nyiginezo. Zaidi ya watu milioni 20 kutoka matabaka tofauti hushiriki katika mjumuiko huu kila mwaka na kutembelea haram tukufu ya Imam Hussein (AS), ambayo ni ya kipekee kwa aina yake, alisema.
Kushiriki katika matembezi ya Arbaeen kuna umuhimu wa kipekee mwaka huu kwa kuzingatia hali ya sasa katika eneo na ulimwengu wa Kiislamu na haja ya kuimarishwa umoja wa Waislamu, aliendelea kusema.
Kwingineko katika matamshi yake, Nazari amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na nafasi muhimu sana katika kufufua matembezi ya Arbaeen baada ya utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein kuyapiga marufuku kwa miongo kadhaa.
Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.
Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.
Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.
3489443