IQNA

Arbaeen 1446

‘Matembezi ya Arbaeen yanaweza kukuza mazungumzo kuhusu itikadi ya Umahdi

23:24 - August 24, 2024
Habari ID: 3479323
IQNA – Mwanazuoni na mtafiti wa Iraq aliangazia nafasi ambayo matembezi ya Arbaeen yanaweza kuwa nayo katika kukuza fikra kuhusu Umahdi yaani itikadi ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake)

Abbas Shamseddin ar-Rabiei amesema matembezi ya kila mwaka ya Arbaeen yanasaidia kueneza fikra ya Umahd duniani na kufikisha ujumbe wake kwa walimwengu.

Mamilioni ya watu wanaoshiriki matembezi ya Arbaeen wanalenga mfungamano wa Arbaeen na Umahdi, alibainisha.

Pia alisema moja ya matunda ya matembezi ya Arbaeen ni kuendeleza makabiliano na dhulma na ukandamizaji kwani matembezi hayo ni sawa na kutangaza upya kila mwaka  utiifu kwa mafundisho ya Ahl-ul-Bayt (AS).

Ama kuhusu mchango wake katika ustaarabu mpya wa Kiislamu, ar-Rabiei amesema ustaarabu wa Kiislamu umeegemezwa kwenye nguzo fulani kama vile maadili na kanuni ambazo nyingi hudhihirika na kuimarishwa katika matembezi ya Arbaeen.

Amesema watu wachamungu na waadilifu hubeba bendera ya Arbaeen na kushikilia kanuni zake na kupitia kwayo wanaimarisha ustaarabu wa Kiislamu.

Kwingineko katika matamshi yake, mwanazuoni huyo wa Iraq aliashiria ujumbe wa mwamko wa Imam Hussein (AS) na kusema ni wa nyakati zote, zikiwemo zama za sasa.

Alisema kwamba kama vile katika Vita vya Karbala, ulimwengu wa leo umegawanyika katika pande mbili: Mrengo wa Haki na Mrengo wa Batili.i

Imam Husein (AS) angewaambia Waislamu leo ​​wahuishe Uislamu, watekeleze mafundisho ya Qur'an kama wokovu wa ulimwengu huu na unaofuata upo katika kufuata mafundisho ya Kitabu Kitukufu, na wasimame dhidi ya madhalimu, alisema.

Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu  wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.

Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika  katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.

Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.

3489624

 

Habari zinazohusiana
captcha