IQNA

Qari wa Misri aibuka mshindi katika Mashindano ya Qur'ani ya Mataifa ya BRICS nchini Brazil

14:56 - September 08, 2025
Habari ID: 3481199
IQNA – Mwakilishi wa Misri ameibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya kimataifa ya usomaji wa Qur'ani ya mataifa ya BRICS yaliyofanyika nchini Brazil.

Waziri wa Wakfu wa Misri, Sheikh Osama Al-Azhari, alituma ujumbe wa pongezi kwa Mohammed Ahmed Fathallah Ahmed kwa mafanikio yake katika mashindano hayo ya kimataifa, kwa mujibu wa tovuti ya Youm7.

Sheikh Al-Azhari alimsifu qari huyo wa Misri, akisema alikuwa mwakilishi stahiki wa taifa lake katika mashindano hayo ya heshima.

Aliwahimiza Mohammed Ahmed na maqari wengine wa Misri kuendeleza njia ya mashindano katika nyanja ya Qur'ani na matendo mema, akisisitiza kuwa Misri bado ni ardhi ya usomaji wa Qur'ani, inayovutia macho ya dunia kwa sauti zake tamu za Qur'ani katika kila pembe ya dunia.

Akizungumzia msaada wa Wizara ya Wakfu kwa vipaji vya Qur'ani, alisema kuwa msaada huo unachangia kukuza kizazi kipya cha wasomaji mahiri “wanaostahiki hadhi ya kidini na ya Qur'ani ya Misri.”

Aliongeza kuwa Mohammed Ahmed Fathallah Ahmed atatuzwa katika hafla rasmi kwa mafanikio yake katika mashindano hayo ya Brazil.

BRICS ni kifupi cha majina ya Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini—mataifa matano yaliyoanzisha umoja huo kupinga ubabe wa Magharibi.

Tuzo ya Pili ya Qur'ani Tukufu ya BRICS ilifanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil, siku ya Ijumaa, tarehe 5 Septemba 2025, siku moja baada ya mkutano wa viongozi wa dini ya Kiislamu kutoka nchi wanachama wa BRICS uliofanyika katika jiji hilo hilo.

BRICS ni kifupi cha majina ya Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini – nchi tano zilizoanzisha umoja huo kwa lengo la kukabiliana na utawala wa kibeberu wa Magharibi.

Mwaka jana BRICS ilipanuka na kujumuisha Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu. BRICS sasa inawakilisha asilimia 45 ya watu duniani, asilimia 25 ya biashara ya kimataifa, asilimia 40 ya uzalishaji wa mafuta duniani na asilimia 28 ya Pato Ghafi la Taifa.

4303813

Habari zinazohusiana
captcha