IQNA

Indonesia kuendeleza msaada kwa shule za Kiislamu licha ya upungufu wa bajeti

15:51 - July 02, 2025
Habari ID: 3480881
IQNA – Serikali ya Indonesia imeahidi kuwa changamoto za bajeti hazitasababisha kusitishwa kwa msaada kwa shule za Kiislamu nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Kidini Indonesia imesisitiza tena azma yake ya kuimarisha huduma na msaada kwa shule za Kiislamu za bweni (maarufu kama vyuo vya mafunzo ya dini – pesantren), licha ya vizingiti vya bajeti na sera ya serikali ya kubana matumizi ya kitaifa.

“Bajeti inaweza kuwa finyu, lakini dhamira yetu haijabadilika,” alisema Endi Suhendi Zen, afisa kutoka Idara ya Pesantren ya wizara hiyo, siku ya Jumanne.

Alibainisha kuwa ni takriban vyuo 5,100 tu kati ya zaidi ya vyuo 42,000 vya Kiislamu vilivyopo nchini Indonesia ndivyo ambavyo tayari vimenufaika na mpango wa ujasiriamali unaotolewa na wizara kupitia Mpango wa Kujitegemea wa Pesantren.

Mwaka huu, inatarajiwa kuwa takriban vyuo 1,000 zaidi vya Kiislamu vitaingizwa kwenye mpango huo.

“Tungependa kusaidia zaidi, lakini tunapaswa kuelewa kuwa bajeti yetu ni ndogo,” Zen alisema kwa unyenyekevu.

Aliwasihi wasimamizi wa vyuo hivyo vya dini kuhakikisha wanakamilisha hatua zote muhimu za kusasisha taarifa zao za taasisi ndani ya mfumo wa Wizara ya Mambo ya Kidini.

Kwa mujibu wa Zen, udhaifu wa usimamizi wa takwimu umekuwa kikwazo kikubwa kwa upatikanaji wa msaada. Vyuo vingi vya Kiislamu havijasasisha taarifa kuhusu wanafunzi, walimu, na miundombinu yao kwa njia ya kidijitali – jambo linaloathiri upangaji wa misaada ya serikali.

“Fedha za serikali mara nyingi hukwama kutolewa kwa sababu takwimu hazijaunganishwa vizuri,” alieleza.

Zen alizipongeza taasisi kadhaa za Kiislamu ambazo zimeweza kujiendeleza kwa njia ya kisasa bila kupoteza asili na utambulisho wao kama taasisi za elimu ya dini ya Kiislamu.

3493686

Kishikizo: indonesia kiislamu
captcha