Tarehe 21 Septemba sasa imetangazwa rasmi kuwa “Siku ya Wadee” katika jimbo la Illinois, ikiwa ni heshima kwa kijana huyo ambaye kifo chake kilizua hisia kote nchini.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika bustani ya Van Horn Woods East Park, Plainfield, ambapo uwanja wa michezo umepewa jina lake, na mnara wa kumbukumbu ulizinduliwa mapema majira ya kiangazi, kwa mujibu wa taarifa ya CBS News.
Hafla hiyo iliwakutanisha jamaa wa Wadee, majirani, wanaharakati, na wawakilishi wa serikali ya jimbo. Viongozi wa jamii walisema kuwa tukio hilo lililenga si tu kuhifadhi kumbukumbu ya Wadee, bali pia kuchochea juhudi pana za kupinga chuki. Mzungumzaji mmoja alimwelezea mtoto huyo kuwa “mwenye moyo uliojaa mapenzi na roho yenye mwangaza.”
Kwa waliokuwepo, siku hiyo ilikuwa na ujumbe mzito. “Leo, kwetu sote, ni ahadi ya kupigania mustakabali ambao Wadee alistahili,” alisema mshiriki mmoja.
Maadhimisho hayo yalijumuisha uchoraji wa moja kwa moja, watoto wakicheza katika uwanja mpya wa michezo, na muziki wa burudani.
Shughuli hiyo iliandaliwa kwa msaada wa Muungano wa Wananchi Waislamu (Muslim Civic Coalition) na Sauti ya Wayahudi kwa Amani (Jewish Voice for Peace), ikiashiria wito wa pamoja wa kustawisha uvumilivu. Wabunge wa jimbo walihudhuria pia, wakibainisha kuwa maadhimisho hayo yaliwezekana kufuatia azimio lililopitishwa mapema mwaka huu na bunge la Illinois.
Wadee Alfayoumi aliuawa mwezi Oktoba 2023 baada ya mwenye nyumba kumvamia yeye na mama yake, akimchoma kisu mara 26.
Mama yake alinusurika, lakini waendesha mashtaka walisema shambulio hilo lilichochewa na chuki dhidi ya Uislamu na lilitokana na kuzuka kwa vita kati ya Israel na Hamas. Mshambuliaji huyo baadaye alihukumiwa kwa kosa la mauaji na uhalifu wa chuki.
“Mtoto huyu aliuawa kwa sababu ya maneno ya chuki na ya kumdhalilisha mwanadamu,” alisema Amina Barhumi kutoka Muungano wa Wananchi Waislamu wakati wa hafla hiyo.
Wengine walizungumza kuhusu athari binafsi za kisa cha Wadee. Samm Costello, aliyesafiri kwa saa mbili kuhudhuria, alisema hajawahi kukutana na Wadee lakini aliguswa sana baada ya kusikia habari zake.
“Sitawahi kusahau athari aliyoacha katika maisha yangu kwa kusikia tu jina lake kwenye taarifa ya habari,” alisema. Costello aliongeza kuwa kumbukumbu ya Wadee imemsukuma kuchukua msimamo. “Macho yangu yamefunguka. Yataendelea kuwa wazi. Nitaendelea kutetea. Nitaendelea kupigania na kuzungumza kwa niaba ya wanaodhulumiwa.”
Maadhimisho hayo yaliangukia siku ya Kimataifa ya Amani, jambo ambalo waandaaji walisema liliongeza uzito wa tukio hilo. Walisisitiza kuwa kila mtoto anastahili kuishi kwa usalama na heshima, na wakaahidi kuendeleza hadithi ya Wadee. Waliongeza kuwa juhudi zaidi za kisheria zinatarajiwa siku za usoni.
3494699