IQNA

Vitendo vya Chuki dhidi ya Uislamu na uharibifu wa chakula katika duka la Pizza Marekani

16:43 - June 07, 2025
Habari ID: 3480803
IQNA – Malalamiko ya ukiukaji wa haki za kiraia yamewasilishwa kwa Idara ya Haki za Kiraia ya Jimbo la Michigan nchini Marekani dhidi ya tawi la Domino’s Pizza lililoko Waterford, kufuatia ripoti ya ubaguzi wa kidini na uharibifu wa chakula uliowalenga wanawake wawili Waislamu na watoto wao.

Tukio hilo lilitokea kutokea jioni ya Machi 11, wakati wanawake hao – ambao ni Wamarekani wenye asili ya Kilebanoni – walipofika dukani kuchukua oda yao ya chakula. Kwa mujibu wa malalamiko hayo, mmoja wa wanawake pamoja na msichana mdogo katika kundi hilo walikuwa wamevaa hijabu, hali iliyodaiwa kumchochea mfanyakazi mmoja wa duka kuonyesha tabia ya uhasama.

Mteja mwingine aliyekuwepo dukani aliwataarifu kuwa mfanyakazi huyo alikuwa ametamka maneno ya matusi na chuki dhidi ya Uislamu. Mmoja wa wanawake hao alipojaribu kumkabili mfanyakazi huyo, hali ya sintofahamu iliongezeka, kwa mujibu wa maelezo katika malalamiko.

Familia hiyo iliporejea nyumbani na kuanza kula chakula, waligundua kuwa mojawapo ya pizza ilikuwa imewekewa nyama ya nguruwe – chakula kilichokatazwa kabisa kwa mujibu wa imani ya Kiislamu. Pia walidai kuwa walikuta unywele uliyopachikwa ndani ya jibini la pizza nyingine.

Familia hiyo iliripoti tukio hilo kupitia tovuti ya makao makuu ya Domino’s na pia kuwasiliana na usimamizi wa duka hilo. Ingawa meneja wa duka na msimamizi wa kanda walikiri kuwa tukio hilo liliripotiwa na wakaahidi kufanya uchunguzi wa ndani, walikana kuwapo kwa makosa yoyote wakidai hakuna ushahidi wa moja kwa moja.

Mbali na malalamiko hayo ya kiraia, wanawake hao waliwasilisha taarifa kwa Idara ya Polisi ya Waterford Township. Polisi tayari wamekamilisha uchunguzi wao na kuwasilisha jalada hilo kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Kaunti ya Oakland kwa ajili ya uamuzi kuhusu iwapo mashtaka ya jinai yafunguliwe. Hadi Jumatatu, ofisi ya mwendesha mashtaka haikuwa imetoa majibu yoyote.

Barua nyingine ilitumwa kwa makao makuu ya Domino’s mwezi Aprili ikiomba uchunguzi rasmi, lakini walalamikaji wanasema hawajapata majibu yoyote hadi sasa.

“Hili si kosa la kawaida wala uzembe wa huduma kwa wateja, bali ni tendo la makusudi la ubaguzi wa kidini lililowadhalilisha na kuwaweka hatarini familia ya Kiislamu,” alisema Dawud Walid, Mkurugenzi Mtendaji wa tawi la Michigan la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), ambalo liliwasilisha malalamiko hayo.

“Tunahitaji kuona uwajibikaji kutoka kwa Domino’s Pizza, na tunaitaka Idara ya Haki za Kiraia ya Michigan kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili la kusikitisha.”

“Malalamiko haya hayaangazii tu suala la chakula kilichoharibiwa,” alisema wakili wa CAIR, Bi. Amy Doukoure. “Yanahusu kuwawajibisha mashirika makubwa yanapofumbia macho au kuendeleza chuki dhidi ya Waislamu waziwazi.”

3493352

Habari zinazohusiana
captcha