IQNA

Mpango wa kubadilisha nakala za zilizochakaa za Qur'ani kwa mpya bila malipo nchini Malaysia

15:13 - September 07, 2025
Habari ID: 3481194
IQNA- Waislamu wa jimbo la Kedah nchini Malaysia wamepata fursa adhimu ya kubadilisha nakala zao za Qur'anI zilizochakaa au kuharibika kwa nakala mpya zilizoidhinishwa rasmi na Wizara ya Mambo ya Ndani bila malipo.

Mpango huu, unaojulikana kama Jom Exchange Quran (JEQ), umefanyika katika banda la wizara hiyo ndani ya Programu ya MADANI Rakyat (PMR) iliyofanyika katika Kituo cha Michezo cha Halmashauri ya Wilaya ya Baling kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2025.

Hamidah Ahmad, afisa msaidizi wa kitengo cha Utekelezaji na Udhibiti wa Wizara, alieleza kuwa mpango huo unalenga kuhifadhi heshima ya Qur'an Tukufu kwa kuhakikisha nakala zilizoharibika zinawekwa mbali kwa mujibu wa taratibu za kidini. Kufikia siku ya pili ya tukio hilo, takriban nakala 200 mpya za Qur'an zilikuwa tayari zimeshatolewa kwa wananchi, huku zaidi ya nakala 500 za zamani zikipokelewa kwa ajili ya kuwekwa mbali kwa njia stahiki.

Mbali na mpango wa kubadilisha nakala za Qur'ani, banda hilo pia lilionyesha machapisho yanayochukuliwa kuwa na maudhui hatarishi au yanayoweza kuathiri maadili ya jamii. Mgeni mmoja, Muhammad Yusof Md Muhyiddin kutoka Bukit Mertajam, Penang, alieleza kuwa banda hilo lilikuwa na manufaa makubwa, si tu kwa kusaidia kutenga kwa njia sahihi nakala zilizochakaa za Qur'an, bali pia kwa kutoa elimu kuhusu machapisho yenye taarifa potofu kuhusu Uislamu.

Mpango huu wa JEQ unatoa mfano bora wa jinsi taasisi za serikali zinavyoweza kushirikiana na jamii kulinda heshima ya maandiko matakatifu, huku zikikuza uelewa wa kijamii na kidini. Ni hatua inayostahili kuigwa na mataifa mengine yanayothamini utukufu wa Qur'an na maadili ya Kiislamu.

3494484

Kishikizo: malaysia qurani tukufu
captcha