Sheikh Nazir Mohamed Ayyad alitoa kauli hiyo katika hafla ya kuwaenzi wahifadhi wa Qur’ani katika Mkoa wa Al-Sharqia nchini Misri.
Amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi Qur’ani Tukufu sambamba na kuitekeleza kwa lengo la kuinua nafsi na kusafisha jamii, hasa katika nyakati za mitihani na changamoto, ambako kuna haja kubwa ya kuzingatia masuala ya kiroho na maadili ili kuongoza maisha na kuelekeza watu kwenye haki na wema.
Aidha, amesema kuwa miongoni mwa malengo makuu ya Qur’ani ni kulinda taasisi ya familia kwa misingi imara ya haki na huruma, na akatilia mkazo kuwa kuwaheshimu wazazi ni miongoni mwa maadili makuu yanayopewa kipaumbele na Qur’ani na dini ya Uislamu kwa ujumla.
Ayyad aliendelea kueleza kwamba kushikamana na mafundisho ya Qur’ani na kutii amri zake ndilo suluhisho bora zaidi la kulinda usalama wa kiroho na kijamii, hasa mbele ya wimbi la mmomonyoko wa maadili na migongano ya fikra inayotishia mshikamano wa jamii.
Amefafanua kuwa “mhifadhi wa kweli wa Qur’ani ni yule anayefanya Qur’ani kuwa mwongozo wake, na anayepima maneno na matendo yake kwa mizani ya mafundisho ya Qur’ani.”
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kuwatunuku vyeti na zawadi wahifadhi wa Qur’ani, ambapo tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii.
3493300