IQNA

Tarouti: Sauti ya Sheikh Sha’sha’i iliwafanya wasikilizaji wahisi Utukufu wa Qur’ani

18:49 - November 14, 2025
Habari ID: 3481512
IQNA – Qari mashuhuri wa Misri, Abdul Fattah Tarouti, amemuelezea marehemu Sheikh Abdul Fattah Sha’sha’i kuwa ni msomaji wa Qur’an aliyebeba sauti ya kipekee na ya kifahari, iliyodhihirisha ukubwa wa Qur’an na kuasisi mtindo wa kipekee wa qira’a.

Akizungumza Jumanne katika mahojiano na kituo cha satelaiti cha Al-Nas kwa kumbukumbu ya kifo cha Sheikh Sha’sha’i, Sheikh Tarouti ambaye ni Naibu Mkuu wa Wasomaji wa Qur’ani wa Misri, alitafakari juu ya urithi wa kudumu wa bwana huyo katika sanaa ya qira’a.

Alisema Sheikh Abdul Fattah Sha’sha’i alikuwa na “sauti yenye haiba na utukufu kiasi kwamba msikilizaji alihisi ukubwa wa Qur’ani, kana kwamba aya zinateremka moja kwa moja kutoka mbinguni.”

Tarouti aliongeza kuwa sauti ya Sha’sha’i “haikupoteza uhai wake kwa miaka yote — iliendelea kuwa safi na yenye ukarimu hadi siku za mwisho za maisha yake.”

Aidha, Tarouti alibainisha kuwa Sha’sha’i alikuwa miongoni mwa wa kwanza kujiunga na Redio ya Misri, jambo lililomjengea nafasi ya pekee katika nyoyo za Waislamu duniani.

Kwa mujibu wa Tarouti, Sha’sha’i alisimama sambamba na Sheikh Muhammad Rif’at na Sheikh Ali Mahmoud kama nguzo za “Enzi ya Dhahabu ya Qira’a” ya Misri.

Alieleza kuwa mtindo wa Sha’sha’i ulikuwa “wa kipekee,” na kwamba wasomaji wachanga wengi leo wanamfuata kwa “uzuri wa utendaji wake na kina cha kiroho katika uwasilishaji wake.”

Tarouti alikumbuka pia kuwa Sha’sha’i ndiye Qari wa kwanza wa Misri kusoma Qur’ani kwa kutumia vipaza sauti katika Msikiti Mtukufu wa Makka na Msikiti wa Mtume Muhammad (SAW) huko Madina, hususan siku ya Arafa, “heshima inayotolewa tu kwa waja walioteuliwa na Mwenyezi Mungu.”

Alimalizia kwa dua ya rehema kwa marehemu Qari, akisema: “Mwenyezi Mungu abariki sauti hii iliyotumikia Qur’ani kwa ikhlasi, na aifanye qira’a yake kuwa nuru kaburini mwake na daraja la kuinuliwa mbele ya Mola.”

Sheikh Abdul Fattah Sha’sha’i alizaliwa Machi 21, 1890 katika kijiji cha Sha’sha, Mkoa wa Monufia, Misri. Alihifadhi Qur’an kabla ya kutimiza miaka kumi chini ya malezi ya baba yake, Sheikh Mahmoud Sha’sha’i. Alijitolea maisha yake yote katika kuitumikia Qur’ani na alifariki Novemba 11, 1962 akiwa na umri wa miaka 72. Anajulikana kama “Nguzo ya Sanaa ya Qira’a,” na aliacha zaidi ya rekodi 400 ambazo bado hurushwa hewani na Redio ya Misri hadi leo.

3495377

Kishikizo: qurani tukufu misri qari
captcha