IQNA

Qari wa Qur'ani

Wakati Qari Al-Saadani wa Misri alipoacha kushirikiana na Redio ya Qur'ani

14:50 - May 03, 2024
Habari ID: 3478765
IQNA: Sheikh Ahmed Suleiman al-Saadani alikuwa qari mashuhuri wa Misri na miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kurekodi kisomo chake.

Aprili 30, tunaadhimisha kumbukumbu ya kifo cha msomaji maarufu wa Qur'ani nchini Misri.

Qari Al-Saadani alizaliwa katika kijiji cha Kafr Barash katika Jimbo la Sharqia nchini Misri mwaka wa 1903. Akiwa na umri mdogo, alikwenda Maktab (shule ya Qur'ani) ya kijiji hicho ambako alihifadhi Qur'ani kikamilifu.

Kisha alihamia Cairo katika miaka ya 1930 ili kujifunza mitindo tofauti ya usomaji wa Qur'ani na riwaya kwa Sheikh Al-Jarisi.

Mwalimu wake alimtambulisha al-Saadani kwa maafisa wa wizara ya wakfu kwa ajili ya kusoma Kurani katika Msikiti wa Imam Al-Shaarani mjini humo.

Umaarufu wa Al-Saadani ulianza kuenea nchini humo baada ya kusoma Quran katika mazishi na kisha akapata kutambulika duniani kote baada ya kisomo chake kutangazwa na redio ya Misri.

Baadaye qiraa yake ilirushwa hewani na vituo vingine vingi vya redio katika ulimwengu wa Kiarabu na kwingineko.

Ilikuwa ni wakati ambapo redio ilikuwa ikipata umaarufu miongoni mwa watu na madola makubwa ya dunia kama Ujerumani, Uingereza na USSR (Shirikisho la Sovieti) yalitaka kuvutia umma katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ndiyo maana vituo vya redio vya London, Berlin na Moscow vilitangaza visomo vya Qur'ani, na mojawapo ya qiraa za mwanzo zilizorushwa hewani katika miji hiyo ni ile ya  al-Saadani.

Al-Saadani aliishi katika zama za maqari  wengi mashuhuri wa Kimisri kama vile Sheikh Mohamed Rif’at, Ali Mahmoud, Ahmed Nida, Mansour Bida, al-Husari, Shaashaei, Mohamed Salama, al-Bahtimi na Ali Hazin.

Alikuwa na njia maalum ya qiraa ya Qur'ani ambayo iliwavutia sana hadhirina na kila alipokwenda kumbi zilijaa tele.

Mshairi wa Kimisri Ahmed Shafiq Kamil alipendezwa sana na visomo vya al-Saadani na qari huyo alirekodi qiraa yake kwa ajili malenga huyo lakini visomo hivyo wakati fulani vilirushwa kwenye Redio ya Quran bila kutaja qari, jambo ambalo lilimkasirisha msomaji. Aliwasilisha malalamishi na kuacha kushirikiana na kituo hicho cha redio hadi kifo chake.

Al-Saadani alifariki Aprili 30, 1976 akiwa na umri wa miaka 73.

 

 

 

3488159

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qari misri
captcha