
Mashindano haya ya 26 yameandaliwa na Taasisi ya Kiislamu ya Japan kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa Waislamu na Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kuhamasisha kuhifadhi na kusoma Qur’ani miongoni mwa Waislamu nchini Japan, kama ilivyoripotiwa na tovuti ya Muslimsaroundtheworld.
Hatua ya awali ya mashindano haya itafanyika kwa njia ya mtandaoni kupitia jukwaa la Zoom tarehe 14 Desemba, huku hatua ya mwisho ikifanyika ana kwa ana katika Msikiti wa Jamia wa Tokyoi na Kituo cha Utamaduni cha Kituruki cha Diyanet kilichoko eneo la Shibuya, tarehe 30 na 31 Desemba 2025.
Usajili utaendelea kwa njia ya kielektroniki hadi tarehe 7 Desemba, na ushiriki unaruhusiwa kwa Waislamu wote wanaoishi Japan bila kujali utaifa, bila gharama yoyote ya kifedha.
Mashindano haya yanajumuisha ngazi mbalimbali kwa watoto hadi umri wa miaka 15, kuanzia kiwango cha usomaji kisichokuwa cha ushindani kwa wale waliokwishahifadhi angalau Surah moja, hadi kiwango cha kuhifadhi Qur’ani yote. Kwa kundi la watu wazima wenye umri wa miaka 16 na kuendelea, ngazi ni kuhifadhi Qur’ani kwa ukamilifu.
Kwa mujibu wa waandaaji, lengo kuu la mashindano haya ni kuimarisha mapenzi ya Qur’ani miongoni mwa washiriki, kuwahimiza kuboresha usomaji wao, na kuimarisha uhifadhi wa Neno la Wahyi.
3495480