IQNA

Shirika moja la Japan laanzisha huduma ya mizigo 'Halal'

18:31 - March 17, 2021
Habari ID: 3473744
TEHRAN (IQNA)- Shirika la kimataifa la usafirishaji mizigo la Nippon Express la Japan limeanzisha huduma mpya ya usafirishaji mizigio ambayo inazingatia mafundisho ya Uislamu na hivyo imepewa anuani ya 'Halal'.

Kwa mujibu wa taarifa, huduma hiyo ambayo awali itakuwa ya ndani ya Japan ilianzishwa Machi nane na itatoa huduma kwa Waislamu takribani 200,000 Japan na pia wafanyabiashara na watalii Waislamu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa huduma hiyo itahakikisha kuwa mizigo hiyo haitachanganywa na mizigo mingine ambayo ambayo yamkini ikapelekea Waislamu wawe na wasiwasi.

Waislamu nchini Japan wanazingatia kwa makini suala la kupata huduma halali na hivyo katika usafirishaji mizigo shirika hilo litahakikisha kuwa Waislamu wanasafirishiwa mizigo yao hasa vyakula kwa kutiliwa maanani mafundisho ya Kiislamu. Shirika hilo linalenga kuhakikisha kuwa vifurishi vya Waislamu havichanganywi na vifurishi vingine ambavyo yamkini vikawa na bidhaa haramu kama vile pombe au nyama ya nguruwe.

Wafanyakazi walio katika kitengo cha Halal cha Nippon Express wanapata mafunzo maalumu kuhusu huduma hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni Japan imeimarisha huduma 'Halal' kwa lengo la kukidhi mahitaji ya Waislamu nchini humo na pia kuwavutia watalii na wafanya biashara Waislamu.

/3960279

Kishikizo: japan halal waislamu
captcha