IQNA

Mfasiri wa Kwanza wa Qur'ani Tukufu kwa Kijapani ​

12:36 - April 12, 2025
Habari ID: 3480528
IQNA-Haj Ryoichi Umar Mita alikuwa mfafsiri wa kwanza wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani. Alizaliwa mwaka 1892 katika mji wa Shimonoseki, Mkoa wa Yamaguchi, kisiwa cha Kyushu, Japan, katika familia ya Kisamurai na Kibuddha.​

Baada ya kuhitimu masomo ya biashara katika Chuo Kikuu cha Yamaguchi mwaka 1916, Mita alisafiri kwenda China ambako alijifunza zaidi kuhusu Uislamu kupitia Waislamu wa nchini humo. Mwaka 1920, aliandika mfululizo wa makala zatizwazo "Uislamu nchini China" zilizochapishwa katika jarida la "Tokyo Kinkiyo". Alivutiwa sana na maisha ya Waislamu wa China na wakati huo alikuwa ameshajifunza lugha ya Kichina vizuri.​

Mwaka 1941, akiwa na umri wa miaka 49, Mita alisafiri hadi msikiti mmoja mjini Beijing, mji mkuu wa China, na kutangaza nia yake ya kuingia Uislamu. Alisilimu na kuchukua jina la Umar Mita.​

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, alirejea Japan mwaka 1945 na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kansai, kisha akawa profesa wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Kyoto. Mwaka 1957, alisafiri kwenda Pakistan na kushiriki katika shughuli mbalimbali za Kiislamu. Mwaka 1960, aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Waislamu wa Japan (JMA) baada ya kifo cha mwenyekiti wa kwanza, Sadiq Imaizumi.​

Katika kipindi chake cha uongozi, aliandika vitabu viwili muhimu kuhusu Uislamu: "Kuelewa Uislamu" na "Utangulizi wa Uislamu", vyote kwa lugha ya Kijapani. Pia alitafsiri kitabu cha "Maisha ya Maswahaba" kilichoandikwa na Muhammad Zakaria kwa lugha ya Kijapani na lugha nyingine za Asia Mashariki.​

Haj Ryoichi Umar Mita alichapisha toleo la kwanza la tarjuma au tafsiri ya Kijapani ya Qur'ani Tukufu tarehe 28 Julai 1972, na toleo lililorekebishwa lilichapishwa mwaka 1982. Baada ya kifo cha mke wake, alijiuzulu kazi yake na kuhamia Tokyo, ambako alijitolea kikamilifu katika kueneza Uislamu. Alifariki dunia mwaka 1983.​

09:24 - 2025/04/12

Wakati wa kuzaliwa kwa Mita, idadi ya Waislamu nchini Japan ilikuwa ndogo sana, lakini baadaye, kutokana na uhamiaji wa Waislamu wengi kutoka Asia ya Kati kama vile Kazakhstan na Tajikistan, pamoja na uhamiaji wa Waislamu kutoka Urusi baada ya Mapinduzi ya Bolshevik katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, maisha ya kijamii ya Waislamu nchini Japan yalianza, na Waislamu walikaa katika miji mikuu ya nchi hiyo.​

Baadhi ya miji nchini Japan iliwakubali Waislamu kama wakimbizi kutoka nchi hizo, na uhusiano wa karibu kati ya Waislamu na watu wa Japan uliimarika. Waislamu walikumbana na matatizo mbalimbali ikiwemo mateso kutoka kwa Wabuddha, lakini Wabuddha waligundua kuwa Waislamu walikuwa watu wa amani, na hivyo uhusiano mzuri uliendelea kuimarika.

3492653

Kishikizo: japan qurani tukufu
captcha