IQNA

Mwanamume akamatwa akiingia Msikiti nchini Marekani akiwa na Bunduki

15:18 - November 22, 2025
Habari ID: 3481552
IQNA – Jeshi la Polisi wa Kaunti ya Richland limethibitisha kukamatwa kwa mwanamume aliyeingia msikiti mmoja wa South Carolina, Marekani, wakati wa sala huku akiwa na bunduki aina ya AR-15.

Tukio hilo lilitokea tarehe 9 Novemba katika msikiti ulioko mjini Columbia. Maafisa wamesema kuwa mtu huyo aliingia ndani wakati wa ibada ya alasiri na kuonekana akizungumza na watoto huku akionesha silaha hiyo. Baadaye, kamera za usalama zilithibitisha mlolongo wa matukio hayo.

Mnamo Jumatano, wachunguzi walitoa picha ya mtuhumiwa. Maafisa walieleza kuwa kijana mwenye umri wa miaka 29, aitwaye Adam White, alijitokeza katika kituo cha polisi siku iliyofuata na kujitambulisha kuwa ndiye mtu aliyeonekana kwenye picha. Alikamatwa muda mfupi baadaye.

White anakabiliwa na mashitaka kadhaa, yakiwemo: kuvuruga sehemu ya ibada, kusababisha taharuki kubwa ya amani, na kuonesha silaha hadharani. Amewekwa katika Kituo cha Kizuizi cha Alvin S. Glenn.

Kukamatwa huku kunakuja wakati taasisi za Kiislamu nchini Marekani zikiripoti ongezeko la hofu za kiusalama. Mashirika ya kitaifa ya haki za kiraia yamebainisha kuongezeka kwa vitisho, uharibifu na unyanyasaji unaolenga misikiti na vituo vya Kiislamu katika miaka ya karibuni.

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni za Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR), matukio hayo yamehusisha vitisho vya silaha, majaribio ya uchomaji moto, na uharibifu wa mali katika majimbo mbalimbali.

3495488

captcha