IQNA

Jinai za Israel

Walowezi wa Kizayuni waweka rekodi mpya katika hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa

21:06 - December 30, 2022
Habari ID: 3476331
TEHRAN (IQNA)- Shirika la Kiislamu linalosimamia masuala ya Msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) linasema kwamba idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni wa Israel walivamia eneo hilo takatifu la Kiislamu mwaka 2022.

Hadi kufikia Disemba 29 2022, walowezi 48,238 wamekiuka eneo hilo, ambalo ni eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu. Hayo yamedokezwa na Azzam Khatib, mkurugenzi wa Idara ya Wakfu ya Kiislamu ambaye amesema kiwango cha ukiukaji dhidi ya msikiti wa Al Aqsa mwaka huu si cha kawaida.

Tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikiwemo al-Quds Mashariki, mwaka 1967, utawala huo umekuwa ukiweka vikwazo dhidi ya haki ya Wapalestina ya kuabudu katika eneo hilo.

Utawala huo ghasibu mara kwa mara hutoa ulinzi kwa hujuma za walowezi hao haramu katika eneo hilo takatifu. Lengo la Wazayuni katika hujuma dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ni kuumiza hisia za kidini za Wapalestina na Waislamu wenzao kote duniani.

Kwa mujibu wa afisa huyo, Waisraeli wenye misimamo mikali wamekuwa wakitumia njia za uchochezi huku wakivamia eneo la Msikiti wa Al Aqsa ikiwa ni pamoja na kutekeleza ibada za Kiyahudi kwenye eneo hilo na kunyanyua bendera ya utawala huo ghasibu.

Khatib amesisitiza kwamba Msikiti wa al-Aqsa ni sehemu takatifu ya Kiislamu na amelitaja eneo hilo kuwa msikiti mtakatifu kwa Waislamu peke yao duniani kote na hawakubali kugawanywa msikiti huo.

Afisa huyo pia ameonya kwamba baraza jipya la mawaziri la serikali ya mrengo wa kulia wa utawala haramu wa Israel -- ambayo ni yenye misimamo mikali zaidi kuwahi kutokea katika historia ya utawala huo -- huenda likatekeleza baadhi ya vitendo vya ukiukaji katika Msikiti wa Al Aqsa ambavyo vinaweza kusababisha vita vya kidini katika eneo na duniani.

3481871

captcha