IQNA

Chama cha Wahudumu wa Qur’ani Chasifu Uchaguzi wa Busara na Hekima wa Kiongozi Mpya

20:33 - March 09, 2026
Habari ID: 3482035
IQNA – Chama cha Wahudumu wa Qur’ani Tukufu nchini Iran kimesifu uamuzi wa busara na hekima wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa kumchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Siku ya Jumatatu, sekretarieti ya Chama cha Wahudumu wa Qur’ani Tukufu cha Iran ilipongeza uamuzi huo.

“Shukrani na sifa zisizo na kikomo zimwendee Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye kwa mara nyingine ameliteremshia neema taifa la Iran linalomtafuta Mungu, kwa kumweka mmoja wa kizazi cha Mtume Muhammad (SAW), kutoka nasaba tukufu ya Ali na Fatimah (amani iwe juu yao) na mwenye asili ya kizazi cha Imam Husayn, katika kiti cha uongozi wa taifa la mapinduzi la Iran na wafuasi wanaotafuta uhuru wa Umma wa Muhammad (SAW),” ilisema sekretarieti hiyo katika taarifa yake.

“Uamuzi wa busara na hekima wa wawakilishi wa taifa walioteuliwa katika Baraza la Wataalamu, katika kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu iliyotajwa katika Qur’ani Tukufu isemayo: ‘Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mrejeshe amana kwa wenye kustahiki…’ (Qur’ani 4:58), umeleta utulivu na faraja kwa watu watukufu wa Iran na kwa wafuasi wote wa Imam wa taifa aliyeuawa kishahidi, huku ukisambaza kukata tamaa na kuvunjika moyo miongoni mwa safu za ukafiri, kiburi cha kimataifa, na wavamizi wa Kizayuni.”

Chama hicho pia kilitangaza utiifu wake wa dhati na wa moyo wote kwa kiongozi huyu mpendwa na mwenye hekima, kikimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amjaalie maisha marefu yenye baraka na mafanikio katika kuendeleza njia ya Imam wa Mapinduzi aliyeuawa kishahidi.

Baraza la Wanazuoni Wataalamu nchini Iran limemchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa Jumapili, tarehe 8 Machi 2026, Baraza hilo lilitoa rambirambi kufuatia kuuawa shahidi Imam Khamenei pamoja na mashahidi wengine waliouawa katika shambulizi la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 28 Februari. Aidha baraza hilo limelaani vikali kwa nguvu zote uvamizi huo wa kinyama wa Marekani mhalifu pamoja na utawala mwovu wa Kizayuni

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mara tu baada ya shahada ya Imam Khamenei, licha ya kuwepo kwa hali ya vita na vitisho vya moja kwa moja kutoka kwa maadui, Baraza la Wanazuoni Wataalamu halikupoteza muda katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, bali lilianza mara moja mchakato wa kumchagua na kumtangaza Kiongozi mpya.

Marekani na utawala wa Israel walianzisha mashambulizi dhidi ya Iran kuanzia asubuhi ya Jumamosi, tarehe 28 Februari.

Kujibu uvamizi huo wa Marekani na Israel uliosababisha kuuawa shahidi Imam Khamenei, pamoja na makamanda kadhaa wakuu wa kijeshi na mamia ya raia wakiwemo wanawake na watoto, Iran ilianzisha Operesheni Ahadi ya Kweli 4 , ikitekeleza mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya malengo ya Israel na vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

4339370

captcha