IQNA

Mpango wa Kuhifadhi Qur’ani Gerezani Kano, Nigeria wazaa matunda

14:34 - May 03, 2026
Habari ID: 3482195
IQNA – Gereza moja huko Wudil, katika jimbo la Kano nchini Nigeria, inasherehekea mafanikio ya kipekee ya kielimu: wafungwa tisa wamekamilisha kuhifadhi Qur’ani Tukufu yote kwa moyo.

Hili linaonyesha kuwa hata mtu akiwa kifungoni, bado anaweza kukua kiroho na kielimu.

Mafanikio haya yamekuja sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Gereza la Wudil.

Afisa wa Uhusiano wa Umma wa Kamandi ya Jimbo la Kano katika Huduma ya Marekebisho ya Nigeria (Nigeria Correctional Service), Musbahu Lawan Kofar Nasarawa, amesema baadhi ya wafungwa hao walipofikishwa gerezani hawakuwa na maarifa makubwa ya usomaji kamili wa Qur’ani, lakini kupitia kujitolea, nidhamu na mafunzo yaliyoandaliwa kwa utaratibu, waliweza kufikia daraja la kuhifadhi Qur’ani yote.

“Yaliyopatikana yanaonyesha dhamira endelevu ya huduma hii katika marekebisho, urekebishaji wa tabia na kuwaandaa wafungwa kurejea tena katika jamii, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Marekebisho ya mwaka 2019,” alisema Kofar Nasarawa.

Aliongeza kuwa kwa miaka mingi, Gereza la Wudil limeendelea kuwa mfano mzuri wa vituo vya marekebisho, kwa kuwapatia wafungwa fursa za elimu, mafunzo ya stadi za kazi pamoja na programu za malezi ya maadili.

Aidha alisema Mdhibiti wa Marekebisho wa Kamandi ya Jimbo la Kano, Ahmed Yusuf Lakpene, alimpongeza Mdhibiti Mkuu wa Huduma ya Marekebisho, Sylvester Ndidi Nwakuche, kwa maelekezo yake yanayohamasisha programu za elimu na mafunzo ya stadi katika vituo vya marekebisho kote nchini.

Amesema mipango kama hiyo ni muhimu katika kuwapa wafungwa ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kurejea katika jamii kwa mafanikio.

Afisa anayesimamia Gereza la Wudil, CSC Ibrahim Wada Ibrahim, pia alishukuru msaada wa Kamandi ya Jimbo, akieleza kuwa mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi bora na dhamira ya kuendeleza na kuwajenga wafungwa.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Aliko Dangote, Wudil, Profesa Musa Tukur Yakasai, aliipongeza Kamandi kwa juhudi zake za kubadilisha maisha ya wafungwa, akisema kuwa mipango ya aina hii ina mchango mkubwa katika kuwawezesha kurejea katika jamii kama wanajamii wema na wenye kuwajibika.

3497310

captcha