IQNA

Wairani washiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds

1:58 - July 11, 2015
Habari ID: 3326322
Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran mwaka huu yamekuwa makubwa na mapana zaidi kuliko miaka iliyopita.

Ijumaa hii mamilioni ya wananchi wa tabaka mbalimbali wameshiriki katika maandamano hayo yaliyofanyika kote nchini wakitetea malengo na mapambano ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel. Waandamanaji katika miji zaidi ya 770 hapa nchini walikuwa wakitoa nara ya Siku ya kimataifa ya Quds, dhihirisho la malengo ya Palestina, umoja wa Umma wa Kiislamu, ujahilia wa kisasa na mauaji ya watoto kuanzia Gaza hadi Yemen. Vilevile walipiga nara za "mauti kwa Marekani", mauti kwa Israel, mauti kwa watawala wa kifalme wa Aal Saud" na mauti kwa matakfiri.
Katika maandamano ya leo ya Siku ya Kimataifa ya Quds, wananchi Waislamu wa Iran walioko katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani wameitaja Palestina kuwa ndilo suala muhimu zaidi la Waislamu kote duniani na wametoa wito wa kuwepo mshikamano wa Umma wa Kiislamu dhidi ya ujahilia wa kisasa na mauaji ya watoto huko Gaza na Yemen.
Maandamano ya leo, kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, pia yamehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu kama Rais Hassan Rouhani na Spika wa Bunge, Dakta Ali Larijani. Rais Rouhani amesema wakati wa maandamano hayo kwamba, Siku ya Kimataifa ya Quds ni siku ya kuonesha mshikamano wa mataifa ya Waislamu na wapigania uhuru kote duniani kwa malengo na mapambano ya Wapalestina. Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, mustakbali uko wazi na kwamba Waislamu wote likiwemo taifa la Palestina, watafikia malengo yao makuu kwa mshikamano, umoja, jihadi na kujitolea. Vilevile amewapongeza wananchi wa Iran kwa kushiriki kwa wingi katika maandamano ya leo ya Siku ya Kimataifa ya Quds.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge Dakta Ali Larijani amesema kuwa kutokana na hali ya sasa ya Mashariki ya Kati utawala wa Kizayuni wa Israel unadhani kuwa umepata uhuru wa kufanya kila kitu na kuendelea kuwakandamiza watu wa Palestina, lakini maandamano ya leo ya Siku ya Kimataifa ya Quds hapa nchini Iran na maeneo mengine duniani yameonesha kuwa, Palestina kamwe haitasahaulika.
Waandamanaji mjini Tehran wametoa azimio lenye vipengee kumi wakisisitiza uungaji mkono wao kwa mapambano ya Kiislamu kuanzia Palestina hadi Yemen. Sehemu moja ya azimio hilo imesema: Taifa la Iran linakutambua kukombolewa Baitul Muqaddas, kibla cha kwanza cha Waislamu, na uhuru wa wananchi wasio na ulinzi wa Palestina kutoka kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni miongoni mwa malengo na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu na stratijia muhimu ya hayati Imam Khomeini na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi Ayatullahil Udhma Ali Khamenei kwa ulimwengu wa Kiislamu na kwamba ndiyo siri ya umoja na mshikamano wa Waislamu.
Azimio hilo limesema: Taifa la Iran linalitambua suala la Palestina, kukombolewa Quds tukufu na juhudi za kufuta kabisa donda la kansa linaloitwa Israel kuwa ni kipaumbele cha kwanza kabisa za Waislamu. Azimio hilo limesema, njia pekee ya kutatua kadhia ya Palestina ni kurejeshwa wakimbizi wa Palestina katika makazi na nchi yao na kuitisha kura huru ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa Palestina.
Azimio hilo la Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran pia limelaani mauaji ya wanawake, watoto wadogo na watu wasio na ulinzi wa Yemen yanayoendelea kufanywa na utawala wa Saudi Arabia na kutahadharisha kuwa, huduma inayotolewa na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa maadui wa Uislamu haitakuwa na matunda kwa watawala vibaraka na tegemezi ghari ya madhila na kushindwa.

3326115

captcha