IQNA

11:33 - September 20, 2018
News ID: 3471681
TEHRAN (IQNA) Mamilioni ya Waislamu, hasa Mashia, wamejitokeza katika maeneo mbali mbali kote duniani kukumbuka tukio chungu la Siku ya Ashura, siku ambayo aliuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS.

Nchini Iran, tokea jana tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram mamilioni ya waumini walijiunga na wenzao kote duniani katika vikao, majlisi na shughuli za maombolezo na kukumbuka misiba na masaibu yaliyomsibu Imam Hussein bin Ali AS ndugu na maswahaba zake waaminifu katika jangwa la Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria.

Kilele cha maombolezo hayo duniani ni katika mji wa Karbala, Iraq iliko Haram Takatifu ya Imam Hussein AS ambapo Wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW na wapenda haki kutoka maeneo yote ya dunia wamejumuika kukumbuka tukio la Ashura. Hafla kubwa za maombolezo pia zinafanyika katika nchi kama vile Lebanon, Syria, Pakistan, India, Uturuki, na miji mingie mikubwa duniani kama vile London, New York, Dar es Salaam, Nairobi na maeneo mengi ya kaskazini mwa Nigeria.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 61 Hijria Qamaria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi kubwa la batili ili kuilinda dini ya Allah.

Katika siku kumi za kwanza za mwezi wa Muharram, Waislamu, hasa wafuasi wa Madhebu ya Shia na wale wawapendao Ahul Bayt wa Mtume SAW, hushiriki katika hafla mbali mbali za maombolezo ya Imam Hussein AS. Aidha hata wasio kuwa Waislamu katika maeneo mbali mbali pia hujumuika na Waislamu katika maombolezo ya Imam Hussein AS kwani aliuawa shahidi akitetea haki na kupinga udhalimu.

3466785

Name:
Email:
* Comment: