IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Pigo la IRGC kwa adhama ya Marekani ni jambo ambalo limepelekea nchi hiyo ifedheheke

19:55 - January 17, 2020
Habari ID: 3472379
THERAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pigo la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kwa adhama ya Marekani ni jambo ambalo limepelekea nchi hiyo ifedheheke na kuongeza kuwa: "Pigo hilo kubwa na lenye nguvu haliwezi kufidiwa kwa chochote na hivyo hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kuongeza vikwazo haiwezi kuondoa fedheha hiyo."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika hotuba za Sala ya Ijumaa ya aina yake mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Kushiriki taifa la Iran katika mazishi ya shahidi mtoharifu Qassem Soleimani na wenzake na pia jibu kali la IRGC lililotolewa kwa kushambulia kituo cha Ainul Assad cha Jeshi la Marekani(nchini Iraq) ni siku mbili ambazo zinaweza kutajwa kuwa Siku za Mwenyezi Mungu (Yaumullah). Siku hizi zimejaa somo na ibra na ni za kuainisha hatima." Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Moja ya njama za kujaribu kufunika siku hizo za Mwenyezi Mungu za wiki za hivi karibuni ni hatua ya serikali khabiti za Ulaya ambazo zimetoa tishio la kuipeleka kadhia ya nyuklia ya Iran mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kwa maana halisi ya neno, nchi za Ulaya  zimedhalilishwa na Marekani na zinautumikia utawala huo wa Washington. Ameongeza kuwa: "Nchi za Ulaya ziko kwenye ndoto ya kuipigisha magoti Iran, lakini ukweli ni kuwa hata bwana wao mkubwa, yaani Marekani, hajaweza kufikia ndoto hiyo seuze wao."

Aidha amesema mazungumzo na nchi za Ulaya yamejaa hadaa na udanganyifu na kuongeza kuwa: "Hawa mabwana wanaokaa katika meza ya mazungumzo kwa hakika  ndio wale wale magaidi wa Uwanja wa Ndege wa Baghdad ambao sasa wamebadilisha mavazi yao."

Ayatullah Khamenei katika sehemu ya pili ya hotuba yake ambayo ameitoa kwa lugha ya Kiarabu ameashiria jinai ya kiuoga ya Marekani kumuua kigaidi jenerali mkubwa na shujaa Muirani na mpigana jihadi Muiraki mwenye kujitolea na mwenye ikhlasi na kuongeza kuwa jinai hiyo imetekelezwa kwa amri ya rais wa Marekani ambaye ni gaidi. Kiongozi Muadhamu amesema: "Hatima ya wazi ya eneo la Asia Magharibi ni kukombolewa kutoka katika satwa ya kibeberu na kiistikbari ya Marekani na kukombolewa Palestina kutoka utawala wa kiajinabi wa Kizayuni na lengo hilo linaweza kufikiwa kwa hima ya mataifa."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasisitizia mataifa yote ya eneo kuwa, "Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuanzisha safu mpya na hisia zilizoamka katika nyoyo za waumini ziamshe ile hisia ya kujiamini miongoni mwa mataifa na wote wafahamu kuwa njia pekee ya kukombolewa mataifa ni kuwa na tadibiri, kusimama kidete na kutomuogopa adui."

3872175

captcha