IQNA

Uturuki yaunga mkono adhabu aliyopata gaidi aliyewaua Waislamu New Zealand

19:02 - August 28, 2020
Habari ID: 3473112
TEHRAN (IQNA) –Idara ya Masuala ya Kidini Uturuki (Dyanet) imepongeza hukumu ya maisha jela iliyotolewa dhidi ya gaidi Muaustralia ambaye alihusika katika mauaji ya Waislamu nchini New Zealand.

Sheikh Profesa Ali Erbas, Mkuu wa Diyanet amesema adhabu hiyo, ambayo ni kali zaidi nchini New Zealand, ni ujumbe wenye nguvu wa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi.

Mahakama Kuu ya New Zealand jana ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa msamaha kwa Brenton Tarrant, mzungu gaidi aliyeungama kuwa na imani ya kujiona bora, ambaye aliwaua kwa kuwapiga risasi Waislamu 51 waliokuwa wakisali katika msikiti miwili ya mji wa Christchurch Machi 15, 2019.

Profesa Erbas ametuma ujumbe katika mitandao ya kijamii na kusema hukumu dhidi ya gaidi huyo imewaridhisha wanaadamu wote.

Halikadhalika Profesa Erbas ametangaza kufungamana na Waislamu wa New Zealand huku akiwamboea maghufira ya Allah SWT wale wote waliopoteza maisha katika hujuma ya kigaidi ya Christchurch.

Tarrant, ambaye ni raia wa Australia, alikiri makosa yake alipofikishwa mahakamani mapema mwaka huu akikabiliwa na mashtaka 51 ya kuua, kujaribu kuua mara 40 na shtaka jengine moja la kufanya kitendo cha kigaidi Machi 2019 katika mji wa kusini mwa New Zealand wa Christchurch huku akionyesha mubashara jinai hizo katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

 Akizungumza mara baada ya kutolewa hukumu hiyo, Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema, amefarajika "kwamba mtu huyo hatauona tena mwanga wa jua." 

3919556

captcha