IQNA

Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu yalaani kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu

21:26 - September 07, 2020
Habari ID: 3473145
TEHRAN (IQNA) - Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu limelaani kitendo cha jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo cha kumvunjia heshima tena Bwana Mtume Muhammad SAW na vile vile kitendo kichafu kilichofanywa nchini Sweden cha kuuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu.

Katika taarifa yake iliyotolewa mapema leo, Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu, yenye makao yake Tehran,imeeleza kuchukizwa na vitendo hivyo vya kijahili na visivyo na mantiki na kutangaza kuwa, kitendo kiovu na kilichorudiwa tena na jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa cha kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW na vile vile kuchomwa moto Msahafu wa nuru ya Qur'ani tukufu nchini Sweden ni mifano hai ya ujahilia mamboleo na upotokaji wa kifikra na wa kiakhlaqi wa zama hizi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kama ambavyo Waislamu walijitolea kukabiliana na watu waliodanganyika kifikra na wenye misimamo ya kufurutu mpaka wa kundi linalojiita ISIS au Daesh, wakapambana kuwahami Wakristo na Waizadi katika nchi za Syria na Iraq; na kama ambavyo pia Hizbullah ya Lebanon inajitoa mhanga kuwalinda wananchi wenzao Wakristo wa nchi hiyo, hivi sasa wakati umewadia kwa wafuasi wa dini za mbinguni, nao pia kutumia mawasilianao ya intaneti na hasa mitandao ya kijamii kutoa jibu mwafaka linaowastahiki wanaoukejeli na kuuvunjia heshima Uislamu.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Baraza la Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu imezitolea mwito taasisi na asasi za kisheria kuchukua hatua madhubuti kulingana na sheria za kimataifa dhidi ya hatua hizo chafu.

Katika maandamano haramu na yasiyo na kibali yaliyofanyika Agosti 28 katika mji wa Malmo nchini Sweden, wafuasi wa kundi moja la mrengo wa kulia lenye misimamo ya kufurutu mpaka lilijusuru kuuchoma moto Msahafu.

Siku ya Jumanne iliyopita pia na katika hatua ya kifidhuli, jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo lilichapisha tena vikatuni vya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW. Aidha watu wanaouchukia Uislamu nchini Norway hivi karibuni nao pia waliivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa kuchana chana kurasa zake na kuzitemea mate.

3921382

captcha