IQNA

Wabunge wa Algeria wawasilisha muswada wa kuharamisha uhusiano na Israel

20:58 - January 08, 2021
Habari ID: 3473536
TEHRAN (IQNA) - Makumi ya wabunge wa Algeria wameandaa muswada wa sheria inayolenga kuufanya kuwa ni uhalifu uanzishwaji wa uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Yousuf Adjissa, mwanachama wa Harakati ya Jamuiya ya Amani, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha Kiislamu nchini Algeria, ameukabidhi muswada huo kwa Rais wa Bunge la nchi hiyo, kwa niaba ya wabunge zaidi ya 50 wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina la Shehab, muswada huo una vipengee saba, na cha kwanza kinasema: Lengo ni kukufanya kuwa ni kosa la uhalifu kuanzisha uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Kipengee hicho kimeeleza kuwa, ni marufuku kuwasiliana, kuanzisha uhusiano wa aina yoyote, au kufungua ofisi za kibalozi za kiwango chochote ile katika utawala wa Kizayuni, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

Kipengee kingine cha muswada huo kinasema, hairuhusiwi kusafiri kwenda au kutoka katika utawala wa Kizayuni, na pia ni marufuku kuingia au kupewa uraia na utawala huo katika ofisi yoyote ile ya kibalozi ya Algeria.

Yousuf Adjissa amesisitiza kuwa, lengo la kutunga sheria hiyo ni kuhakikisha pia kwamba kufanya biashara au miamala yoyote ya kiuchumi na utawala wa Kizayuni pamoja na mashirika ya utawala huo haramu kunahesabiwa kuwa ni kosa la uhalifu.

Hatua hiyo inakuja wakati ambao mwaka wa 2020, nchi nne za Kiarabu ambazo ni Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco zilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na hivyo kujiunga na Misri na Jordan ambazo zinautambua utawala huo ghasibu.

Inaaminika kuwa Saudi Arabia nayo tayari ina uhusiano wa siri na utawala haramu wa Israel lakini inahofia kuutangaza uhusiano huo hadharani utaharibu sura yake kabisa katika ulimwengu wa Kiislamu.

3473635

captcha