IQNA

Hamas yapongeza azimio la Baraza la Usalama la UN la kusimamisha vita Gaza

18:25 - June 11, 2024
Habari ID: 3478961
IQNA -Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imepokea vizuri kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio ambalo limeunga mkono mpango unaolenga kuleta usitishaji mapigano katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.
Hamas imesema imelikubali azimio hilo katika taarifa iliyotoa kwa vyombo vya habari jana Jumatatu, saa chache baada ya baraza hilo lenye wanachama 15 kupiga kura kwa wingi za kuliunga mkono.
Azimio hilo lililowasilishwa na Marekani limeungwa mkono na nchi 14 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama, ukiondoa Russia ambayo imejizuia kupiga kura.
 
Katika taarifa yake, Hamas imesema imeyapokea vizuri yaliyomo kwenye azimio la Baraza la Usalama ambayo yanazungumzia kwa dhati usitishaji wa kudumu wa mapigano huko Ghaza, kuondoka kikamilifu majeshi ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo na kutekelezwa ubadilishanaji wa mateka. 

Taarifa hiyo vilevile imesema, harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imeidhinisha vifungu vingine vya mpango huo, ambavyo ni kuhusu kujengwa upya Ukanda wa Ghaza, kurejea makwao Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao, kukataliwa kufanywa mabadiliko yoyote ya kidemografia ya idadi ya watu au kupunguzwa kwa eneo la Ghaza, na ufikishwaji wa misaada inayohitajika kwa watu wa ukanda huo.

 
Taarifa hiyo ya Hamas imebainisha "utayari" wa harakati hiyo "kutoa ushirikiano kwa wapatanishi kwa ajili ya kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja juu ya kutekeleza misingi inayoendana na matakwa ya Wapalestina na Muqawama.
 
Kwa mara ya kwanza tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha vita vya umwagaji damu na mauaji ya kimbari dhidi ya Waplestina wa Ghaza miezi minane iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hatimaye limeidhinisha usitishaji mapigano wa haraka, hata hivyo maswali mengi yamebaki juu ya utekelezaji wake.
3488696
captcha