IQNA

Sheikh Zakzaky ni mtetezi wa Nigeria iliyoungana

20:37 - July 04, 2021
Habari ID: 3474070
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) imesema kiongozi wa harakati hiyo aliye gerezani, Sheikh Ibrahim Zakzaky, daima amekuwa akipigania Nigeria iliyoungana kama taifa moja.

Taarifa iliyotolewa Jumamosi imesema Sheikh Zakzaky amekuwa daima ni mtetezi wa Nigeria moja na hata amekuwa akiunga mkono shirikisho la pamoja la Nigeria na nchi zote jirani ili mataifa yote yaweze kunufaika na utajiri wa kiutamaduni na mali asili.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya kuanzishwa kampeni potovu katika mitandao ya jamii Nigeria ambayo imemlinganisha Sheikh Zakzaky Nnamdi Kanu na Sunday Igboho ambao ni vinara wa makundi yanaotaka kujitenga baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Hayo yanajiri siku moja baada ya Mahakama ya Nigeria kwa mara nyingine tena kuakhirisha kikao cha kusikilizwa kesi ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN), Sheikh Ibrahim Zakzaky hadi tarehe 28 Julai licha ya Waislamu wa nchi hiyo kutaka mwanazuoni huyo aachiwe huru.

Mahakama Kuu ya Jimbo la Kuduna imetangaza kuwa, imechukua uamuzi huo ili kutoa fursa ya kuchukuliwa maamuzi kuhusu faili hilo na kwamba, faili lenyewe lilikuwa bado halijafikishwa kwenye mahakama hiyo. Hata hivyo mshauri wa Sheikh Zakzaky amekadhibisha madai hayo akisema faili la kesi yake lilikuwa tayari limekabidhiwa mahakamani. 

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake, Mallimah Zeenah walitiwa nguvuni tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria na amekuwa mahabusu kwa kipindi chote cha miaka 6 iliyopita. Mahakama ya Kaduna imekuwa ikikataa ama kumhukumu au kumuachia huru, na mara zote inatoa visingizio vya aina mbalimbali vya kuhalalisha kuendelea kumshikilia mahabusu. 

Mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia yameongezeka sana hususan baada ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya IMN. Mikusanyiko ya kidini ya wafuasi wa kiongozi huyo imepigwa marufuku, na askari usalama wanakabiliana kwa mkono wa chuma na maandamano au mkusanyiko wowote wa Waislamu hao. Kwa maneno mengine ni kuwa, serikali ya Abuja imefanya jitihada za kuwazuia kabisa Waislamu kushiriki katika harakai zote za kisiasa na kijamii nchini humo. 

3981919

captcha