IQNA

Yemen yasubiri jibu la Umoja wa Mataifa kuhusu mpango mpya wa kumaliza mapigano

11:20 - August 18, 2021
Habari ID: 3474204
TEHRAN (IQNA)- Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen linasema linasubiri majibu chanya kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mjumbe wake mpya wa Yemen, Hans Grundberg, kuhusu mpango uliopendekezwa na Harakati ya Ansarullah kwa ajili ya kusaidia kumaliza vita nchini Yemen.

Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, limesema katika taarifa iliyochapishwa Jumatatu, kwamba linasubiri jibu la Umoja wa Mataifa kuhusu hatua zilizopendekezwa na Kiongozi wa Ansarullah Abdul-Malik Badreddin al-Houthi kuhusu kusitisha mapigano kitaifa.

Taarifa hiyo ilisema mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen hapaswi kufumbia macho mzingiro wa kinyama dhidi ya Yemen ambao umekuwa ukitekelezwa na utawala  vamizi wa Saudia na waitifaki wake.

Baraza hilo vile vile limeulaumu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kutokana na kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika majimbo ya Yemen, haswa huko Hudaydah na maeneo mengine ya pwani.

Saudi Arabia huku ikiungwa mkono kwa hali na mali na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani, utawala wa Kizayuni, Uingereza na nchi kadhaa nyingine kama vile Sudan, mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha mashambulizi ya kijeshi ya pande zote dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu nchi hiyo maskini ya Kiarabu. 

Hadi sasa makumi ya maelfu ya Wayemen wameshauawa katika vita hivyo vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, huku makumi ya maelfu wakijeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. 

Mwezi Julai,Kituo cha sheria na maendeleo cha A'inul-Insaaniyyah kilichoko mji mkuu wa Yemen Sana'a kilitangaza kuwa, idadi ya wahanga wa jinai zilizofanywa na muungano wa Saudia katika muda wa siku 2,300 zimefika watu 43,891 waliouawa shahidi na waliojeruhiwa, kwa upande wa raia wa kawaida.

Kituo hicho kimeongeza kuwa, katika kipindi hicho cha vita, raia 17,176  wakiwemo watoto 3,842 na wanawake 2,400 wameuawa na wengine 26,715 wakiwemo watoto 4,225 na wanawake 2,832 wamejeruhiwa.

3475518

captcha