IQNA

Hamas yatoa wito kwa Wapalestina kuulinda msikiti wa Al Aqsa

18:26 - September 06, 2021
Habari ID: 3474263
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina ,kwa kifupi Hamas, katika mji wa Quds Tukufu ametoa mwito kwa Wapalestina kujitokeza kwa wingi katika Msikiti wa al-Aqsa ili kuuhami na kuulinda dhidi ya uvamizi wa Walowezi wa Kizayuni, wakati wa sherehe na matambiko yao.

Mohammad Hamadeh alitoa mwito huo jana Jumapili na kuongeza kuwa, hujuma za Walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Msikiti huo mtakatifu zinafanyika kwa mpangilio, utaratibu na vile vile kwa himaya ya polisi na jeshi la utawala huo pandikizi.

Amekumbusha kuwa, mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) ulipo Masjidul Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na moja ya maeneo matatu muhimu zaidi matakatifu ya Kiislamu.

Msemaji wa HAMAS katika mji wa Quds amewaasa Wapalestina kuigeuza siku kuu ya Wazayuni kuwa 'Siku ya Ghadhabu' iwapo Msikiti wa Aqsa utashambuliwa. 

Waumini 45,000 walihudhuria Sala ya Ijumaa iliyopita katika Msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel, huku Wapalestina wengine wengi wakizuiliwa kufika katika eneo hilo takatifu.

Katika miezi ya hivi karibuni, askari wa utawala haramu wa Israel wamekuwa wakisambazwa kandokando ya msikiti wa al-Aqsa na kuweka vituo vya upekuzi ili kuwazuia vijana wa Kipalestina wasiingie msikitini humo.

Msikiti wa al-Aqsa umegeuzwa kuwa eneo la kutamba na kujifaragua askari wa utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni wanaochukua hatua zinazolenga kuubadilisha utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa mji wa Quds (Jerusalem) na badala yake kuufanya kuwa na nembo za Uzayuni.

3475642

Kishikizo: aqsa hamas israel palestina
captcha