IQNA

Wapalestina washukuru serikali ya Iraq kwa kupinga uanzishwaji uhusiano na Israel

20:40 - September 28, 2021
Habari ID: 3474355
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwa mara nyingine tena imeishukuru serikali, makundi ya kisiasa, wazee wa koo na viongozi wa makabila ya Iraq, kwa msimamo wao wa kupinga kuanzishwa mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Msemaji wa Hamas Fawzi Barhum amesema, misimamo ya Iraq inabainisha uungwana wa nchi hiyo ndugu, mapenzi na upendo wake kwa piganio tukufu la Palestina na wananchi wake.

Barhum amesisitiza kuhusu upinzani wa Wapalestina dhidi ya aina yoyote ya uanzishaji uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na akayatolea mwito mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na wafanya mapatano sambamba na kufanya juhudi za kuliwezesha taifa la Palestina kuwa thabiti na endelevu katika kukabiliana na ukaliaji wa mabavu wa ardhi yake.

Juzi Jumapili, Hazem Qassim, msemaji mwengine wa Hamas alitoa taarifa ya kusifu na kupongeza msimamo wa serikali ya Iraq wa kutetea malengo matukufu ya Palestina na kupinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Siku ya Ijumaa, lilifanyika kongomano la kuunga mkono kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel mjini Arbil katika eneo la Kurdistan ya Iraq, kongamano ambalo lililaaniwa na kupingwa vikali na wananchi na shakhsia wa kisiasa na kidini wa nchi hiyo.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na kundi moja la viongozi wa makabila ya magharibi mwa Iraq na baadhi ya viongozi wa utawala uliopinduliwa wa Kibaathi.

Vyombo vya mahakama vya Iraq vimetoa waranti wa kukamatwa washiriki wa kongamano hilo la Arbil.

4000964

captcha