IQNA

Waumini tisa wauawa katika hujuma ya kigaidi Msikitini Nigeria

23:45 - December 10, 2021
Habari ID: 3474662
TEHRAN (IQNA)-Waumini tisa wameuawa katika hujuma ya magaidi dhidi ya msikiti nchini Nigeria katika jimbo la Niger.

Mkuu wa polisi katika jimbo hilo Bala Kuryas amewaambia waaandishi habari kuwa hujuma hiyo ilijiri Jumatano.

Wakaazi wa eneo hilo idadi ya waliouawa si tisa kama ilivyotangazwa na polisi bali ni watu 16 waliouawa na wengine 12 walijeruhiwa katika hujuma hiyo.

Imearifiwa kuwa  washambuliaji waliuvamia msikiti huo mapema Jumatano wakati waumini walikuwa wakijitayarisha kwa ajili ya Sala ya Alfajiri.

Jimbo la Nigeri limekuwa likishuhudia hujuma za magaidi na wezi wa mifugo kwa miaka kadhaa ambapo mamia wameuawa na maelfu yaw engine wameachwa bila makao.

Serikali ya jimbo hilo inasema katika kipindi cha miaka miwili watu 151,000 wameachwa bila makao kutokana na hujuma za magaidi na wezi wa mifugo.

Waislamu wa kaskazini na kaskazini mashariki na kati mwa Nigeria wamekuwa wakilengwa kwa muda mrefu na magaidi wakufurishaji wa Boko Haram ambao huwakufurisha Waislamu wote wasiokubaliana  itikadi zao potovu. Misikiti na shule za Waislamu wasioafikiana na Boko Haram hulengwa mara kwa mara na kundi hilo la kigaidi.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa, ambayo inatumiwa na aghalabu ya Waislamu wa Nigeria, lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad. Halikadhalika ugaidi huo wa Boko Haram umepelekea Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria kubakia nyuma kimaendeleo na hivyo kuathiri vibaya mustakabali wao. Serikali ya Nigeria pia inalaumiwa kwa kuzembea katika kukabiliana namagaidi hao huku kukiwa na ripoti kuwa baadhi ya majenerali jeshini na maafisa wa serikali wanaofaidika na ugaidi huo wa Boko Haram.

4019874/

captcha