Maandamano ya kitaifa pia yamepangwa siku hiyo hiyo mjini Paris, yakianza saa 8 mchana katika Place de l’Université na kuelekea Place de la République.
Wito huo wa kushiriki umetolewa kufuatia kile waandaaji wamedai kuwa ni hali inayoongezeka ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa. Katika tahariri waliyoandika, waliotia saini walihimiza wananchi kushiriki maandamano hayo kuenzi kumbukumbu ya Aboubakar Cissé, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Aprili 25 nje ya msikiti wa Grand-Combe. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Cissé alilengwa “kwa sababu alikuwa Muislamu.”
“Uhalifu huu si tukio lililotokea kwa bahati mbaya. Sio hadithi ya kulipizana kisasi au ugomvi uliomalizika kwa maafa. Ni hadithi ya nchi ambapo mtu mmoja anaamua kumuua mwingine, ambaye hamfahamu, kwa sababu tu anasali msikitini,” ilisomeka taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa waliotia saini, jukumu la tukio hilo halibaki kwa mtu aliyefanya kitendo pekee. Wamesema kuwa mazingira ya kijamii na kisiasa kwa ujumla yamechangia kukuza chuki. “Aliyeua anawajibika. Lakini anayeua kwa misingi ya ubaguzi daima anafanya hivyo ndani ya mazingira yanayochochea,” taarifa iliendelea, ikieleza jukumu la serikali ya Ufaransa katika kuruhusu kuenea kwa hali ya chuki dhidi ya Waislamu, na nguvu ya kisiasa ya chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally.
Waliotia saini pia walikosoa sehemu ya vyombo vya habari vya Ufaransa, wakivituhumu baadhi ya vituo na wachambuzi kwa kuendeleza dhana zenye madhara.
Walitaja “vyombo vya habari vinavyoshikilia misimamo dhidi ya Uislamu,” wakirejelea “vipindi vya matusi kwenye CNews” na wasomi” wanaojificha nyuma ya kauli za kupinga misimamo mikali na hivyo kuonesha chuki dhidi ya Waarabu na watu Weusi.
Wameeleza hofu kuwa baadhi ya watu na taasisi zinazotoa rambirambi juu ya kifo cha Cissé leo hii, awali zilichangia mazingira yaliyowezesha tukio kama hilo kutokea.
Wito huo umehimiza ushiriki wa umma kwa wingi katika maandamano ya kitaifa “kupinga aina zote za ubaguzi wa rangi.”
Mashirika na watu binafsi wanaounga mkono maandamano haya ni pamoja na Collective Against Islamophobia in Europe (CCIE), April 21 March against Racism, Islamophobia, and for the Protection of Children, Urgence Palestine, na Adama Committee. Miongoni mwa watu mashuhuri waliotia saini ni mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi Annie Ernaux, mwanafalsafa Frédéric Lordon, mwandishi Françoise Vergès, msanii Blanche Gardin, na Michèle Sibony kutoka French Jewish Union for Peace (UJFP).
3493005