Olivier Hadzovic, ambaye alimchoma kisu Aboubakar Cissé aliyekuwa na umri wa miaka 22, raia wa Mali, katika msikiti wa La Grande-Combe mnamo Aprili 25, alirejeshwa kutoka Italia siku ya Ijumaa baada ya kujisalimisha kwa mamlaka za huko.
“Mshukiwa alikaa kimya wakati wa kuhojiwa kwake kwa mara ya kwanza mbele ya jaji wa uchunguzi,” alisema mwendesha mashtaka wa Nîmes, Cécile Gensac. Aliongeza kuwa anatarajiwa kuhojiwa tena katika hatua nyingine.
Wakili wa Hadzovic, Adrien Gabeaud, alisisitiza kuwa ukimya wa mteja wake “haupaswi kufasiriwa kama juhudi za kuzuia uchunguzi.” Gabeaud alisema ataiomba mahakama kuruhusu tathmini mbalimbali za kitaalamu, zikiwemo za afya ya akili.
Waendesha mashtaka wanasema Hadzovic alitenda kwa makusudi, na alimpiga picha Cissé wakati akipoteza maisha huku akitoa matusi ya chuki dhidi ya dini.
Mashtaka hayo yanakuja siku chache kabla ya maandamano ya kitaifa yaliyopangwa kufanyika Jumapili, Mei 11, kwa heshima ya Cissé. Mkutano mkuu utafanyika jijini Paris, huku maandamano sawia yakitarajiwa katika miji mingine kote Ufaransa. Mikutano hiyo inaandaliwa na vikundi vya kisiasa, wanaharakati, wasomi na watu mashuhuri kwa lengo la kulaani chuki dhidi ya Uislamu na kumuenzi marehemu.
Mwili wa Cissé ulirejeshwa hivi karibuni nchini Mali kwa maziko, kufuatia tukio hilo ambalo limezua hasira na kusababisha wito mpya wa kuchukua hatua kali dhidi ya uhalifu unaotokana na chuki za kidini.
3493030